Sura 4

1 Wakati Petro na Yohana walipokuwa wakizungumza na watu, makuhani na nahodha wa hekalu na masadukayo waliwajia. 2 Walikuwa wameudhika sana kwa sababu Petro na Yohana walikuwa wanafundisha watu na kutangaza katika Yesu ufufuo kutoka kwa wafu. 3 Waliwakamata na kuwaweka gerezani hadi asubuhi iliyofuata, kwani tayari ilikuwa jioni. 4 Lakini watu wengi waliokuwa wamesikia ujumbe waliamini; na idadi ya wanaume waliokuwa wameamini walikuwa kama elfu tano. 5 Hata ilipofika asubuhi siku iliyofuata, kwamba wakuu wao, wazee na waandishi, kwa pamoja walikusanyika Yerusalemu. 6 Anasi yule kuhani mkuu alikuwepo, na Kayafa, na Yohana, na Iskanda, na wote waliokuwa ni ndugu wa kuhani mkuu. 7 Walipokuwa wamewaweka Petro na Yohana katikati yao, waliwauliza, "Kwa uwezo gani, au kwa jina gani mmefanya hili?" 8 Kisha, Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akawaambia, "Ninyi watawala wa watu, na wazee, 9 kama tunahojiwa siku ya leo kuhusu tendo jema lililofanywa kwa mtu huyu mgonjwa, na kwa namna gani mtu huyu aliponywa, 10 acha lijulikane kuwa hilo kwenu na kwa watu wote katika Israel kwamba huyu mtu ambaye anasismama mbele yenu akiwa mwenye afya kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye mlimsulubisha, lakini ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. 11 Yesu Kristo ni jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikata lakini ambalo limefanywa kuwa jiwe kuu la pembeni. 12 Hakuna wokovu katika mtu mwingine yeyote yule, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa watu, ambalo kwa hilo tunaweza kuokolewa." 13 Sasa walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na wakagundua kwamba walikuwa ni watu wakawaida, wasio na elimu, walishangaa, wakafahamu kwamba Petro na Yohana wamekuwa pamoja na Yesu. 14 Kwa sababu walimwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuwa na kitu cha kusema dhidi ya hili. 15 Lakini baada ya kuwa walipokuwa wamewaamuru mitume waondoke mbele ya mkutano wa baraza, walizungumza wao kwa wao. 16 Walisema, tuwafanyeje watu hawa? Ni kweli kwamba muujiza wa ajabu umefanyika kupitia wao unajulikana na kila mmoja anayeishi Yerusalemu, na hatuwezi kulikataa hilo. 17 Lakini, ili kwamba jambo hili lisienee miongoni mwa watu, acha tuwaonye wasinene tena kwa mtu yeyote kwa jina hili. 18 Hatimaye waliwaita Petro na Yohana ndani na kuwaamuru kamwe wasinene wala kufundisha kwa jina la Yesu. 19 Lakini Petro na Yohana walijibu na kuwaambia, "Kama ni sahihi machoni pa Mungu kuwatii ninyi kuliko Mungu, hukumuni wenyewe. 20 Maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo ambayo tumeyaona na kuyasikia." 21 Baada ya kuwaonya sana Petro na Yohana, waliwaacha waende. Hawakuweza kupata sababu yoyote ya kuwaadhibu, kwa sababu watu wote walikuwa wakimsifu Mungu kwa kile kilichokuwa kimetendeka. 22 Yule mtu aliyekuwa amepokea muujiza wa uponyaji alipata kuwa na umri zaidi ya miaka arobaini. 23 Baada ya kuwaacha huru, Petro na Yohana walikuja kwa watu wao na wakawapasha habari yote ambayo makuhani wakuu na wazee walikuwa wamewaambia. 24 Walipoyasikia, walipaza sauti zao kwa pamoja kwa Mungu na kusema, "Bwana, wewe uliyeumba mbingu na dunia na bahari na kila kitu ndani yake, 25 Wewe ambaye ulinena kwa Roho Mtakatifu kupitia kwa kinywa cha mtumishi wako, baba yetu Daudi, 'Kwanini watu wa mataifa wamefanya ghasia, na watu wametafakari mambo yasiyofaa?' 26 Ulisema, wafalme wa dunia wamejipanga pamoja, na watawala wamekusanyika kwa pamoja dhidi ya Bwana, na dhidi ya Masihi wake." 27 Ni hakika, wote Herode na Pontio Pilato, pamoja na watu wa mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika kwa pamoja katika mji huu dhidi ya mtumishi wako mtakatifu Yesu, ambaye ulimpaka mafuta. 28 Walikusanyika kwa pamoja kufanya yote ambayo mkono na mpango wako uliamua tangu awali, yangefanyika. 29 Sasa, Bwana, yaangalie matisho yao, na ukawajaalie watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri wote. 30 Nyoosha mkono wako kuponya, ishara na maajabu viweze kutokea kupitia jina la mtumishi wako mtakatifu Yesu." 31 Baada ya kuwa wamemaliza kuomba, eneo walipokuwa wamekusanyika pamoja likatikiswa, na wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, na kunena neno la Mungu kwa ujasili. 32 Idadi kubwa ya wale walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja wao aliyesema kwamba chochote alichomiliki kilikuwa cha kwake mwenyewe, badala yake walikuwa na vitu vyote shirika. 33 Kwa nguvu kubwa mitume walikuwa wakiutangaza ushuhuda wao kuhusu ufufuo wa Bwana Yesu, na neema kubwa ilikuwa juu yao wote. 34 Hapakuwa na mtu yeyote miongoni mwao aliyepungukiwa na chochote, kwa sababu watu wote waliokuwa na hati za viwanja au nyumba, waliviuza na kuleta pesa ya vitu walivyokuwa wameuza 35 na kuviweka chini ya miguu ya mitume, na viligawanywa kwa kila mmoja kulingana na mahitaji yao. 36 Yusufu, mlawi, mtu kutoka Kipro, alipewa jina la Barnaba na mitume (hiyo ikitafsiriwa, ni mwana wa kutia moyo). 37 Aliliuza shamba lake, na akaleta fedha, akaziweka chini ya miguu ya mitume.