Sura 5

1 Sasa mtu mmoja aliyeitwa Anania, na Safira mkewe, waliuza sehemu ya mali, 2 na akaficha sehemu ya fedha waliyouza (mke wake pia alilijua hili), na akaleta sehemu iliyobakia na kuiweka kwenye miguu ya mitume. 3 Lakini Petro akasema, "Anania, kwa nini shetani ameujaza moyo wako kumdanganya Roho Mtakatifu na kuficha sehemu ya mali ya shamba? 4 Wakati lilipokuwa halijauzwa, halikuwa ni mali yako, na baada ya kuuzwa, halikuwa chini ya mamlaka yako? Ilikuwaje uwaze jambo hili moyoni mwako? Hujawadanganya wanadamu, bali umemdanganya Mungu." 5 Kwa kusikia maneno haya, Anania alidondoka chini na akakata roho, na hofu kubwa iliwajia wote waliolisikia hili. 6 Vijana wakaja mbele na wakamfunga sanda, na kumpeleka nje na kumzika. 7 Baada ya masaa matatu hivi, mke wake aliingia ndani, asijue ni nini kilichokuwa kimetokea. 8 Petro akamwambia, "Niambie, kama mliuza shamba kwa thamani hiyo." Akasema, "Ndiyo, kwa thamani hiyo." 9 Kisha Petro akamwambia, "Inakuwaje kwamba mmekubaliana kwa pamoja kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu ya wale waliomzika mme wako iko mlangoni, na watakubeba na kukupeleka nje." 10 Ghafla akaanguka miguuni pa Petro, akakata roho, na wale vijana wakaja ndani wakamkuta ameshakufa. Wakambeba kumpeleka nje, na kumzika karibu na mmewe. 11 Hofu kubwa ikaja juu ya kanisa zima, na juu ya wote walioyasikia mambo haya. 12 Ishara nyingi na maajabu yalikuwa yanatokea miongoni mwa watu kupitia mikono ya mitume. Walikuwa pamoja katika ukumbi wa Sulemani. 13 Lakini, hakuna mtu mwingine tofauti aliyekuwa na ujasiri wa kujiunga nao; hata hivyo, walipewa heshima ya juu na watu. 14 Na pia, waamini wengi walikuwa wakiongezeka kwa Bwana, umati mkubwa wa wanaume na wanawake, 15 kiasi kwamba hata waliwabeba wagonjwa mitaani, na kuwalaza vitandani na kwenye makochi, ili kwamba Petro akiwa anapita, kivuli chake kiweze kushuka juu ya baadhi yao. 16 Hapo pia, idadi kubwa ya watu walikuja pamoja kutoka miji iliyozunguka Yerusalem, wakiwaleta wagonjwa na wote waliopagawa na roho wachafu, na wote waliponywa. 17 Lakini kuhani mkuu aliinuka, na wote waliokuwa pamoja naye (ambao ni wa dhehebu la masadukayo); na walijawa na wivu 18 na wakanyosha mikono yao kuwakamata mitume na kuwaweka ndani ya gereza la jumla. 19 Hata hivyo wakati wa usiku malaika wa Bwana akaifungua milango ya gereza na kuwaongoza nje na kusema, 20 "Nendeni, mkasimame hekaluni na kuwaambia watu maneno yote ya uzima huu." 21 Waliposikia hili, waliingia hekaluni wakati wa kupambazuka na kufundisha. Lakini, kuhani mkuu alikuja na wote waliokuwa naye, na kuita baraza lote kwa pamoja, na wazee wote wa watu wa Israeli, na kuwatuma gerezani ili kuwaleta mitume. 22 Lakini watumishi waliokwenda, hawakuwakuta gerezani, walirudi na kutoa taarifa, 23 "Tumekuta gereza limefungwa vizuri salama, na walinzi wamesimama langoni, lakini tulipolifungua, hatukuona mtu ndani." 24 Sasa wakati nahodha wa hekalu na makuhani wakuu waliposikia maneno haya, waliingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu nini kingeliwatokea kutokana na hilo. 25 Ndipo mtu mmoja akaja na kuwaambia, "Watu mliowaweka gerezani wamesimama hekaluni na wanafundisha watu." 26 Hivyo jemedari alienda pamoja na watumishi, na kuwarudisha, lakini bila ya machafuko, kwa sababu waliwaogopa kwamba watu wangeweza kuwapiga kwa mawe. 27 Walipokwisha kuwaleta, waliwaweka mbele ya baraza. Kuhani mkuu aliwahoji 28 akisema, "Tuliwaamuru msifundishe kwa jina hili, na bado mmeijaza Yerusalemu kwa fundisho lenu, na kutamani kuleta damu ya mtu huyu juu yetu." 29 Lakini Petro na mitume wakajibu, "Lazima tumtii Mungu kuliko watu. 30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, mliyemuua kwa kumtundika juu ya mti. 31 Mungu alimwinua juu katika mkono wake wa kuume, na kumfanya kuwa Mkuu na Mwokozi, kutoa toba kwa Israeli, na msamaha wa dhambi. 32 Sisi ni mashahidi wa mambo haya, na Roho Mtakatifu, ambaye Mungu amemtoa kwa wale wanaomtii." 33 Wajumbe wa baraza waliposikia hivi, walishikwa na hasira wakataka kuwaua mitume. 34 Lakini pharisayo aliyeitwa Gamalieli, mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, alisimama na kuwaamuru mitume watolewe nje kwa muda mfupi. 35 Kisha akawaambia, "Wanaume wa Israeli, iweni makini sana na kile mnachopendekeza kuwafanyia watu hawa. 36 Kwa sababu, zamani zilizopita, Theuda aliinuka na kujidai kuwa mtu mkuu, na idadi ya watu, wapata mia nne walijiunga naye. Aliuawa, na wote waliokuwa wakimtii walitawanyika na kuwa si kitu. 37 Baada ya mtu huyu, Yuda mgalilaya, aliinuka siku zile za kuandikwa sensa, akavuta watu wengi nyuma yake. Naye pia aliangamia na wote waliokuwa wakimtii walitawanyika. 38 Sasa nawaambia, jiepusheni na watu hawa na muwaache wenyewe, kwa sababu, kama mpango huu au kazi hii ni ya wanadamu, itatupwa. 39 Lakini kama ni ya Mungu, hamtaweza kuwazuia; mnaweza mkajikuta hata mnashindana na Mungu." Hivyo, walishawishika. 40 Kisha, waliwaita mitume ndani na kuwachapa na kuwaamuru wasinene kwa jina la Yesu, na wakawaacha waende zao. 41 Waliondoka mbele ya baraza wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuteseka na kutoheshimiwa kwa ajili ya Jina hilo. 42 Kwa hiyo, kila siku, ndani ya hekalu na kutoka nyumba kwa nyumba waliendelea kufundisha na kutangaza habari njema kwamba Kristo ni Yesu.