Sura 25

1 Ndipo Festo alipoingia katika jimbo hilo na baada ya siku tatu alienda toka Kaisaria hadi Yerusalemu. 2 Kuhani mkuu na Wayahudi maarufu walileta mashtaka dhidi ya Paulo kwa Festo, na walizungumza kwa nguvu kwa Festo. 3 Na walimwomba Festo kibali dhidi ya Paulo apate kumwita Yerusalemu ili waweze kumuua njiani. 4 Lakini Festo alijibu kwamba Paulo alikuwa mfungwa katika Kaisaria, na kwamba yeye mwenyewe atarudi huko haraka. 5 "Kwa hiyo, wale ambao wanaweza, inawapasa kwenda huko na sisi. Kama kuna kitu kibaya kwa mtu huyu, mnapaswa kumshtaki." 6 Baada ya kukaa siku nane au kumi zaidi, akarudi Kaisaria, na siku iliyofuata akakaa katika kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe kwake. 7 Alipofika, Wayahudi kutoka Yerusalemu wakasimama karibu, Wakatoa mashtaka mengi mazito ambayo hawakuweza kuyathibitisha. 8 Paulo alijitetea na kusema, 'Si sijatenda dhambi dhidi ya sheria ya Wayahudi, au ya hekalu, au dhidi ya Kaisari.' 9 Lakini Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi, na hivyo akamjibu Paulo kwa kusema, 'Je, unataka kwenda Yerusalemu na kuhukumiwa na mimi kuhusu mambo haya huko?' 10 Paulo alisema, 'ninasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari ambapo napaswa kuhukumiwa. Sijawakosea Wayahudi, kama wewe ujuavyo vema. 11 Ikiwa nimekosa na kama nimefanya kinachostahili kifo, sikatai kufa. Lakini kama shutuma zao si kitu, hakuna mtu anayeweza kunikabidhi kwao. Ninakata rufaa kwa Kaisari. ' 12 Baada ya Festo kuongea na baraza akajibu, " umekata rufaa kwa Kaisari. Kwa Kaisari utaenda." 13 Baada ya siku kadhaa, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisaria kufanya ziara rasmi kwa Festo. 14 Baada ya kukaa hapo kwa siku nyingi, Festo aliwasilisha kesi ya Paulo kwa mfalme; Akasema, 'Mtu mmoja aliachwa hapa na Feliki kama mfungwa. 15 Nilipokuwa Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walileta mashtaka juu ya mtu huyu kwangu, nao waliuliza juu ya hukumu dhidi yake. 16 Mimi niliwajibu kwamba haikuwa desturi ya Warumi kumtoa mshitakiwa yeyote kabla hajapata fursa ya kuwakabili washitaki wake na kujitetea dhidi ya tuhuma zao zinazomkabili. 17 Kwa hiyo, walipokuja pamoja hapa, sikuweza kusubiri, lakini siku iliyofuata niliketi katika kiti cha hukumu na kuamuru mtu huyo aletwe ndani. 18 Wakati washitaki waliposimama kumshtaki, niliona kwamba mashataka yao hayakuonyesha uovu wowote. 19 Badala yake, walikuwa na mabishano fulani pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu Yesu ambaye alikuwa amekufa, lakini Paulo anadai kuwa yu hai. 20 Nilikuwa nimetatanishwa jinsi ya kuchunguza suala hili, na nikamwuliza kama angeenda Yerusalemu kuhukumiwa kuhusu mambo haya. 21 Lakini wakati Paulo amekata rufaa kuwekwa chini ya ulinzi kwa ajili ya uamuzi wa Mfalme, niliamuru akae chini ya ulinzi hata nitakapompeleka kwa Kaisari. ' 22 Agripa alimwambia Festo, "ningependa pia kumsikiliza mtu huyu." "Festo, akasema, "kesho utamsikiliza." 23 Hivyo kesho yake, Agripa na Bernike walifika na shamrashamra nyingi; walifika katika ukumbi na maafisa wa kijeshi, na watu mashuhuri wa mji. Na Festo alipotoa amri, Paulo aliletwa kwao. 24 Festo akasema, "Mfalme Agripa, na watu wote ambao wapo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu; jumuiya yote ya Wayahudi walikata rufaa kwangu huko Yerusalemu na hapa pia, na wakapiga kelele kwangu kwamba asipate kuishi. 25 Naliona kwamba hakufanya lolote linalostahili kifo; lakini kwa sababu alikata rufaa kwa Mfalme, niliamua kumpeleka Rumi. 26 Lakini sina kitu dhahiri cha kuandika kwa Mfalme. Kwa sababu hii, nimemleta kwako, hasa kwako wewe, Mfalme Agripa, ili nipate kuwa na kitu cha kuandika kuhusu kesi. 27 kwa kuwa naona haina maana kumpeleka mfungwa na bila kuonyesha mashitaka yanayomkabili.