Sura 26

1 Hivyo, Agripa akamwambia Paulo, `Unaruhusiwa kujitetea. ' Ndipo Paulo akanyoosha mkono wake akajitetea hivi. 2 "Najiona mwenye furaha, Mfalme Agripa, ili kufanya kesi yangu mbele yako leo ​​dhidi ya mashtaka yote ya Wayahudi. 3 Hasa, kwa sababu wewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na maswali. Hivyo naomba unisikilize kwa uvumilivu. 4 Kweli, Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu ujana wangu katika taifa langu na huko Yerusalemu. 5 Wananijua tangu mwanzo na wanapaswa kukubali kwamba niliishi kama Mfarisayo, dhehebu lenye msimamo mkali kwenye dini yetu. 6 Sasa nimesimama hapa nihukumiwe kwa sababu ya tumaini langu katika ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa mababa zetu. 7 Hii ni ahadi ambayo makabila yetu kumi na mbili yanatumaini kupokea kama wakimwabudu Mungu kwa bidii usiku na mchana, na ni kwa ajili ya tumaini hili, mfalme, kwamba Wayahudi wananishitaki. 8 Kwa nini ingepasa yeyote kati yenu afikiri ni ajabu kwamba Mungu hufufua wafu? 9 Sasa ni kweli, mimi mwenyewe nilifikiria kwamba ningepisa kufanya mambo mengi dhidi ya jina la Yesu wa Nazareti. 10 Nilifanya haya katika Yerusalemu. Niliwafunga grezani watu wengi watakatifu wa Mungu, kwa mamlaka niliyoipokea kutoka kwa wakuu wa makuhani; na wakati walipokuwa wameuawa, nilipiga kura dhidi yao. 11 Mara nyingi niliwaadhibu katika masinagogi yote na nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Nilikuwa na hasira sana juu yao na niliwatesa hata katika miji ya ugenini. 12 Wakati nilipokuwa nikifanya haya, nilienda Dameski, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu; 13 nilipokuwa njiani wakati wa mchana, Mfalme, niliona mwanga kutoka mbinguni uliokuwa mkali kuliko jua na uling'aa kutuzunguka mimi na watu waliokuwa wakisafiri pamoja nami. 14 Sisi sote tulipoanguka chini, nalisikia sauti ikizungumza na mimi ikisema katika lugha ya Kiebrania: `Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo. 15 Ndipo nikasema, 'Wewe ni nani, Bwana?' Bwana akajibu, 'Mimi ni Yesu ambaye unanitesa. 16 Sasa inuka usimame kwa miguu yako; sababu kwa kusudi hili mimi nimeonekana kwako, nimekuteua kuwa mtumishi na shahidi juu ya mambo ambayo unajua kuhusu mimi sasa na mambo nitakayokuonyesha baadaye; 17 na Nitakuokoa kutoka kwa watu na watu wa Mataifa ambapo ninakutuma, 18 kufungua macho yao na kuwatoa gizani kwenda kwenye mwanga na kutoka kwenye himaya ya shetani wamgeukie Mungu, ili kwamba wapate kupokea kutoka kwa Mungu msamaha wa dhambi na urithi ambao nimewapa wale amabao wametakaswa kwa imani ndani yangu. 19 Kwa hiyo, mfalme Agripa, sikukiuka; maono ya mbinguni, 20 lakini, kwa wale walio katika Dameski kwanza, na kisha Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine, nilihubiri kwamba watubu na kumgeukia Mungu, wafanye matendo yanayostahili toba. 21 Kwa sababu hii Wayahudi walinikamata hekaluni, wakajaribu kuniua. 22 Kwa hiyo nilipokea msaada ambao watoka kwa Mungu hata siku hii ya leo, na ninasimama na kushuhudia kwa watu wa kawaida na wakuu juu ya yale ambayo manabii na Musa walisema yangetokea--- 23 kwamba Kristo lazima ateseke, na kwakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu na kutangaza nuru kwa watu wetu na kwa mataifa. 24 Alipokuwa Paulo amemaliza kujitetea, Festo alisema kwa sauti kubwa, 'Paulo, wewe ni mwendawazimu! masomo yako yamekufanya mwendawazimu. 25 Lakini Paulo akasema, Mimi si mwendawazimu, mheshimiwa Festo, lakini ninatangaza maneno ya ukweli na hukumu ya kweli. 26 Kwa kuwa mfalme anajua kuhusu mambo haya; na hivyo, ninaongea kwa ujasiri kwake, kwa maana nina hakika kwamba hakuna lolote lililofichwa kwake; kwa kuwa hili halijafanywa pembeni. 27 Je, unaamini manabii, Mfalme Agripa? Najua kwamba unaamini. ' 28 Agripa akamwambia Paulo, 'Kwa muda mfupi unaweza kunishawishi mimi na kunifanya Mkristo? 29 Paulo akasema, '"Namwomba Mungu kwamba, iwe kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu, bali pia wote wanaonisikia leo, wawe kama mimi, lakini bila ya minyororo hii ya gereza." 30 Ndipo mfalme alisimama, na liwali, na Bernike pia, na wale waliokuwa wamekaa pamoja nao, 31 walipoondoka ukumbini, walizungumza wao kwa wao na kusema, 'Mtu huyu hastahili kifo wala kifungo.' 32 Agripa akamwambia Festo, "Mtu huyu angeweza kuwekwa huru kama asingekata rufaa kwa Kaisari."