Sura 13

1 Sasa katika kanisa la Antiokia, palikuwa na baadhi ya manabii na walimu. Walikua Barnaba, Simeoni (aliyeitwa Nigeri), Lukio wa Kirene, Manaeni( ndugu asiye wa damu wa Herode kiongozi wa mkoa), na Sauli. 2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu alisema, "Nitengeeni pembeni Barnaba na Sauli, kuifanya kazi ambayo nimewaitia." 3 Baada ya Kanisa kufunga, kuomba, na kuweka mikono yao juu ya watu hawa, wakawaacha waende zao. 4 Kwa hiyo Barnabas na Sauli, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu waliteremka kuelekea Seleukia; kutoka huko walisafiri baharini kuelekea kisiwa cha Kipro. 5 Walipokuwa katika mji wa Salami, walilitangaza neno la Mungu katika Masinagogi ya Wayahudi. Pia walikuwa pamoja na Yohana Marko kama msaidizi wao. 6 Walipokuwa wamepita katika kisiwa chote mpaka Pafo, walimkuta mtu fulani mchawi, Myahudi nabii wa uongo, ambaye jina lake lilikuwa Bar Yesu. 7 Mchawi huyu alishirikiana na Liwali Sergio Paulus, aliyekuwa mtu mwenye akili. Mtu huyu aliwaalika Barnaba na Sauli, kwa sababu alihitaji kusikia neno la Mungu. 8 Lakini Elima "yule mchawi" (hivyo ndivyo jina lake lilivyo tafsiriwa) aliwapinga; alijaribu kumgeuza yule liwali atoke kwenye imani. 9 Lakini Sauli aliyeitwa Paulo, alikuwa amejazwa na Roho Mtakatikfu, akamkazia macho 10 na akasema "Ewe mwana wa Ibilisi, umejazwa na aina zote za udanganyifu na uovu. Wewe ni adui wa kila aina ya haki. Hautakoma kuzigeuza njia za Bwana, zilizonyooka, je utaweza? 11 Sasa tazama, mkono wa Bwana upo juu yako, na utakuwa kipofu. Hautaliona Jua kwa muda" mara moja ukungu na giza vilianguka juu ya Elima; alianza kuzunguka pale akiomba watu wamwongoze kwa kumshika mkono. 12 Baada ya liwali kuona kilichotokea, aliamini, kwa sababu alishangazwa kwa mafundisho kuhusu Bwana. 13 Sasa Paulo na rafiki zake walisafiri majini kutoka Pafo na wakafika Perge katika Pamfilia. Lakini Yohana aliwaacha na kurudi Yerusalemu. 14 Paulo na rafiki yake walisafiri kutoka Perge na wakafika Antiokia ya Pisidia. Huko walikwenda katika sinagogi siku ya Sabato na kukaa chini. 15 Baada ya kusoma sheria na manabii, viongozi wa sinagogi aliwatumia ujumbe wakisema, "Ndugu, kama mnao ujumbe wa kuwatia moyo watu hapa, useme." 16 Kwa hiyo Paulo alisimama na kuwapungia mkono; alisema, "Wanaume wa Israeli nanyi mnaomtii Mungu, sikilizeni. 17 Mungu wa hawa watu wa Israeli aliwainua baba zetu na kuwafanya watu wengi walipokaa katika nchi ya Misri, na kwa mkono wake ulioinuliwa aliwaongoza nje yake. 18 Kwa takribani miaka arobaini aliwavumilia katika jangwa. 19 Baada ya kuyaharibu mataifa saba katika nchi ya Kaanani, aliwapa watu wetu nchi yao iwe urithi. 20 Matukio haya yote yalitokea zaidi ya miaka mia nne na hamsini. Baada ya haya yote, Mungu aliwapa waamuzi mpaka Nabii Samweli. 21 Ndipo watu waliomba kwa ajili ya mfalme, na Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila la Benjamini, kuwa mfalme kwa miaka arobaini. 22 Kisha baada ya Mungu kumuondoa katika ufalme, alimwinua Daudi kuwa mfalme wao. Ilikuwa ni kuhusu Daudi kwamba Mungu alishuhudia na kusema, 'Nimempata Daudi mwana wa Yese kuwa mtu atakayeandama moyo wangu; afanyaye kila kitu nipendacho.' 23 Kutoka kwenye ukoo wa mtu huyu Mungu ameiletea Israeli mkombozi, Yesu, kama alivyoahidi kufanya. 24 Kabla ya Yesu kuja, Yohana kwanza alitangaza ubatizo wa toba kwa watu wote wa Israeli. 25 Naye Yohana alipokuwa akimalizia kazi yake, alisema, 'Mwanifikiri mimi kua ni nani? Mimi si yule. Lakini sikilizeni, ajaye nyuma yangu, sisitahili kulegeza viatu vya miguu yake.' 26 Ndugu, watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wale ambao kati yenu mnamwabudu Mungu, ni kwa ajili yetu kwamba ujumbe huu wa ukombozi umetumwa. 27 Kwa wale waishio Yerusalemu, na watawala wao, hawakumtambua kwa uhalisia, na wala hawakuutambua ujumbe wa manabii ambao husomwa kila Sabato; kwa hiyo walitimiliza ujumbe wa manabii kwa kumhukumu kifo Yesu. 28 Ijapokuwa hawakupata sababu za adhabu ya kifo ndani yake, walimwomba Pilato amuue. 29 Walipokua wamekamilisha mambo yote yaliyoandikwa kuhusu yeye, walimshusha kutoka mtini na kumlaza kaburini. 30 Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu. 31 Alionekana kwa siku nyingi kwa wale waliokwenda pamoja naye kutoka Galilaya kuelekea Yerusalemu. Watu hawa sasa ni mashahidi wa watu. 32 Hivyo tunawaabia habari njema: Kuhusu ahadi walizopewa mababu zetu. 33 Mungu ametutimizia ahadi hizi kwetu, watoto wao, kwa kumfufua Yesu. Kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili: 'Wewe ni Mwanangu, leo nimekuwa Baba yako' 34 Kuhusu kumfufua kutoka kwa wafu, ni kwamba Mwili wake usiharibike tena, amesema namna hii: nitakupa baraka halisi na takatifu alizoahidiwa Daudi' 35 Hii ndiyo sababu amesema pia katika zaburi nyingine, 'Hautaruhusu mtakatifu wako kuuona uozo.' 36 Kwa kuwa baada ya Daudi kutumikia mapenzi ya Mungu katika kizazi chake, alilala, alilazwa pamoja na baba zake, na mwili wake uliona uaharibifu, 37 Lakini aliyefufuliwa na Mungu hakuuona uharibifu. 38 Hivyo na ifahamike kwenu, ndugu, kupitia mtu huyu, msamaha wa dhambi umehubiriwa. 39 Kwa yeye kila aaminiye anahesabiwa haki na mambo yote ambayo sheria ya Musa isingewafanya wenye Haki. 40 Hivyo basi kuweni waangalifu kwamba kitu walichokiongelea manabii kisitokee kwenu: 41 'Tazama, enyi mnaodharau, na mkashangae na mkaangamie; kwa vile nafanya kazi katika siku zenu, Kazi ambayo hamwezi kuiamini, hata kama mtu atawaeleza." 42 Wakati Paulo na Barnaba wakiondoka, watu wakawaomba waongee maneno haya siku ya Sabato iliyofuata. 43 Wakati mkutano wa sinagogi ulipokwisha, Wayahudi wengi na waongofu thabiti waliwafuata Paulo na Barnaba, ambao waliongea nao na waliwahimiza waendelee katika neema ya Mungu. 44 Sabato iliyofuata, karibu mji mzima ulikusanyika kusikia neno la Mungu. 45 Wayahudi walipoona makutano, walijawa na wivu na kuongea maneno yaliyopinga vitu vilivyosemwa na Paulo na walimtukana. 46 Lakini Paulo na Barnaba waliongea kwa ujasiri na kusema, "Ilikuwa ni muhimu kwamba neno la Mungu linenwe kwanza kwenu. Tunapowaona mnalisukumia mbali kutoka kwenu nakujiona kuwa hamkusitahili uzima wa milele, angalieni tutawageukia Mataifa. 47 Kama ambavyo Bwana ametuamuru, akisema, 'Nimewaweka ninyi kama nuru kwa watu wa mataifa, kwamba mlete wokovu kwa pande zote za dunia." 48 Mataifa waliposikia hili, walifurahi na kulitukuza neno la Bwana. Wengi waliochaguliwa kwa uzima wa milele waliamini. 49 Neno la Bwana lilienea nchi ile yote. 50 Lakini wayahudi waliwachochea waliojitoa na wanawake muhimu, pia na viongozi wa mji. Haya yalichochea mateso dhidi ya Paulo na Barnaba na waliwatupa nje ya mipaka ya mji. 51 Lakini Paulo na Barnaba walikung'utia vumbi ya miguu yao. Kisha walienda kwenye mji wa Ikonia. 52 Na wanafunzi walijawa na furaha pamoja na Roho mtakatifu.