Sura 11

1 Sasa mitume na ndugu wale waliokuwa huko Yudea walisikia kuwa watu wa mataifa wamelipokea neno la Mungu. 2 Petro alipokuwa amepanda kwenda huko Yerusalemu, lile kundi la watu waliotahiriwa wakaanza kumkosoa; 3 Walisema, "Wajihusisha na watu wasiotahiriwa na kula nao!" 4 Lakini Petro alianza kuwaeleza tukio kwa kina; akisema, 5 "Nilikuwa naomba katika mji wa Yafa, na nikaona maono ya chombo kikishuka chini kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni katika pembe zake zote nne. Kikashuka kwangu. 6 Nilikitazama na kufikiri juu yake. Nikaona wanyama wenye miguu minne waishio katika nchi, na wanyama wa porini na wanyama watambaao na ndege wa angani. 7 Kisha nikasikia sauti ikisema nami, 'Amka, Petro; chinja na ule!' 8 Nikasema, 'Siyo hivyo, Bwana; kwa maana mdomoni mwangu hakujawahi kuingia kitu chochote kisicho kitakatifu au kichafu' 9 Lakini sauti ikajibu tena kutoka Mbinguni, 'kile ambacho Mungu amekitakasa, usikiite najisi'. 10 Hii ilitokea mara tatu, na kisha kila kitu kikachukuliwa mbinguni tena. 11 "Tazama, wakati huo watu watatu walikuwa wamesimama mbele ya nyumba ile tulimokuwa; walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kuja kwangu. 12 Roho akaniamuru niende pamoja nao, na nisijitofautishe nao. Hawa ndugu sita wakaenda na mimi, na tuliende kwenye nyumba ya mtu yule. 13 Alituambia vile alivyomwona malaika amesimama ndani ya nyumba yake akisema, 'Watume watu Yafa wakamlete simoni ambaye jina lake lingine ni Petro. 14 Atasema ujumbe kwako katika huo utaokoka-- wewe na nyumba yako yote.' 15 Nilipoanza kusema nao, Roho Mtakatifu akaja juu yao kama vile alivyokuja kwetu mwanzoni. 16 Nikakumbuka maneno ya Bwana, alivyosema, 'Yohana alibatiza kwa maji kweli; lakini ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.' 17 Basi ikiwa Mungu aliwapa karama ile ile kama aliyotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, Mimi nilikuwa nani, kwamba ningeweza kumpinga Mungu?" 18 Waliposikia mambo haya, hawakujibu chochote, bali walimtukuza Mungu na kusema, "Basi Mungu amewapa toba ya uzima kwa watu wa mataifa pia." 19 Basi wale waliokuwa wametawanyika kwa mateso yaliyotokea kwa sababu ya Stephano, walienea hadi mpaka Foinike, Kipro na Antiokia, wakilihubiri neno ila kwa Wayahudi peke yao. 20 Lakini baadhi yao, watu kutoka Kipro na Krene, walikuja Antiokia na kusema na Wayunani na kuwahubiria injili kuhusu Bwana Yesu. 21 Na mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, na idadi kubwa ya watu waliamini na kumgeukia Bwana. 22 Habari kuwahusu zilifika masikioni mwa kanisa la Yerusalem na wakamtuma Barnaba aende mpaka Antiokia. 23 Alipokuja na kuona neema ya Mungu alifurahi na aliwatia moyo wote kudumu katika Bwana kwa kusudi la moyo. 24 Kwa sababu alikuwa mtu mwema, na amejaa Roho Mtakatifu na imani, na watu wengi wakaongezeka kwa Bwana. 25 Baadaye Barnaba alienda Tarso kumtafuta kwa umakini Sauli. 26 Alipompata, akamleta Antiokia. Ikawa kwamba, kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa kwanza Wakristo huko Antiokia. 27 Sasa katika siku hizi manabii wakashuka kutoka Yerusalemu mpaka Antiokia. 28 Mmoja wao, ni Agabo kwa jina , akasimama na kuonyeshwa na Roho kuwa njaa kubwa ingetokea duniani kote. Hii ilitokea wakati wa siku za Klaudio. 29 Kwa hiyo, wanafunzi, kila mmoja alivyofanikiwa, waliamua kupeleka misaada kwa ndugu walioko Uyahudi. 30 Walifanya hivi; Walituma pesa kwa mkono wa Barnaba na Sauli.