Sura 10

1 Sasa palikuwa na mtu fulani katika mji wa Kaisaria, jina lake aliitwa Kornelio, alikuwa mkuu wa kikosi cha askari wa Kiitaliano. 2 Alikuwa mtu, aliyemcha Mungu pamoja na nyumba yake yote, alitoa sadaka nyingi kwa watu na kumwomba Mungu siku zote. 3 Muda wa saa tisa za mchana, aliona wazi katika maono Malaika wa Mungu akija kwake. Malaika akamwambia "Kornelio!" 4 Kornelio akatazama malaika na akaogopa sana akasema, "kuna nini bwana?" Malaika akamwambia "Maombi yako na zawadi zako kwa masikini zimepanda juu kama kumbukumbu kwenye uwepo wa Mungu". 5 Sasa tuma watu kwenda mji wa Yafa kumleta mtu anayeitwa Simoni ambaye pia huitwa Petro. 6 Anakaa na mtengenezaji wa Ngozi aitwaye Simoni ambaye nyumba yake iko kando ya bahari." 7 Baada ya Malaika aliyekuwa akisema naye kuondoka, Kornelio akawaita wawili wa watumishi wa nyumbani mwake, na askari mcha Mungu kutoka miongoni mwao waliokuwa wanamtumikia. 8 Kornelio aliwaambia yote yaliyotokea na akawatuma Yafa. 9 Sasa siku iliyofuata muda wa saa sita walipokuwa katika safari yao, nao walikuwa wakiukaribia mji, Petro alipanda juu darini kuomba. 10 Yeye basi akawa na njaa na alihitaji kitu cha kula, lakini wakati watu walipokuwa wanapika chakula, akaonyeshwa maono, 11 akaona anga limefuguka na chombo kinashuka, kitu fulani kama nguo kubwa ikishuka chini kwenye ardhi, chini kwa pembe zake nne. 12 Ndani yake kulikuwa na aina zote za wanyama wenye miguu minne na watambaao juu ya ardhi, na ndege wa angani. 13 Tena sauti ikasema kwake "Amka, Petro chinja na ule". 14 Lakini Petro akasema "Siyo hivyo, Bwana kwa sababu sijawahi kula kitu chochote kilichonajisi na kichafu. 15 Lakini sauti ikaja kwake tena kwa mara ya pili "Alichokitakasa Mungu usikiite najisi wala kichafu". 16 Hii ilitokea mara tatu, na kile chombo kikawa kimechukuliwa tena angani. 17 Na wakati Petro akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa juu ya hayo maono aliyokuwa ameyaona yanamaanisha nini, Tazama, watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakasimama mbele ya lango, baada ya kuuliza njia ya kuwaleta kwenye nyumba. 18 Waliita na kuuliza kama Simoni ambaye pia aliitwa Petro kama alikuwa anakaa pale. 19 Wakati huo Petro alipokuwa akiwaza juu ya hayo maono, Roho akasema naye, "Tazama watu watatu wanakutafuta. 20 Amka na ushuke chini na uende nao. Usisite kwenda nao, kwa sababu nimewatuma." 21 Petro akashuka chini kwao na kusema "Mimi ni yule mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?" 22 Wakasema, "Akida mmoja jina lake Kornelio, mtu mwenye haki na anayemcha Mungu, na watu humsema vyema katika taifa lote la Kiyahudi, aliagizwa na malaika mtakatifu kukutuma kwako uende nyumba kwake, ili asikie ujumbe kutoka kwako." 23 Hivyo Petro akawakaribisha kuingia ndani na kukaa pamoja naye. 24 Siku iliyofuata walikuja Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwasubiri; na alikuwa amewaita pamoja ndugu zake na marafiki zake wa karibu. 25 Ikawa kwamba wakati Petro aliingia ndani, Kornelio alikutana naye na kuanguka chini miguuni pake ili kumwabudu. 26 Lakini Petro akamwinua na kusema "Simama! Mimi mwenyewe pia ni mwanadamu." 27 Wakati Petro akiwa anaongea naye, alienda ndani akakuta watu wengi wamekusanyika pamoja. 28 Akawaambia, "Ninyi wenyewe mnajua kuwa si halali kwa Myahudi kushirikiana na au kumtembelea mgeni. Lakini Mungu amenionyesha mimi kuwa sipaswi kumwita mtu yeyote najisi au mchafu. 29 Na ndiyo maana nimekuja bila kubishana, nilipoitwa. Hivyo nakuuliza kwa nini ulituma nije." 30 Kornelio akasema, "Siku nne zilizopita, wakati kama huu, nilikuwa naomba muda wa saa tisa mchana ndani ya nyumba yangu; na tazama, mtu alisimama mbele yangu mwenye mavazi yenye kung'aa. 31 Akasema 'Kornelio maombi yako yamesikiwa na Mungu, na zawadi zako kwa masikini zimemkumbusha Mungu juu yako. 32 Hivyo tuma mtu Yafa na akamwite mtu mmoja anayeitwa Simoni aje kwako, ambaye pia huitwa Petro. Anaishi kwa mtengenezaji mmoja wa ngozi mmoja aitwaye Simoni ambaye nyumba yake iko ufukweni mwa bahari'. 33 Kwa hiyo mara moja nilikutuma uje. Wewe ni mwema umekuja. Sasa basi, sisi sote tupo hapa mbele za Mungu kusikia kila kitu ambacho umeangizwa na Bwana kusema." 34 Ndipo Petro akafungua mdomo wake na kusema "Kweli, nimeelewa kuwa Mungu hawezi kuwa na upendeleo. 35 Badala yake, katika kila taifa mtu yeyote anayemwogopa na kufanya matendo ya haki anakubalika kwake. 36 Unajua ujumbe alioutoa kwa watu wa Israel, alipokuwa akitangaza habari njema ya amani kupitia Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote- 37 ninyi wenyewe mnajua tukio lililotokea, ambalo limetokea Yudea yote, kuanzia Galilaya, baada ya ubatizo ambao Yohana alitangaza. 38 Tukio lililokuwa linamhusu Yesu Kristo wa Nazareti jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na kwa nguvu. Alienda akifanya mema na kuponya wote walioteswa na ibilsi, kwa kuwa Mungu alikuwa pamoja naye. 39 Sisi ni mashahidi wa mambo yote Yesu aliyoyafanya katika nchi za Wayahudi na katika Yerusalemu. Walimuua kwa kumtundika juu ya mti, 40 Lakini Mungu alimfufua siku ya tatu na kumfanya aonekane, 41 si kwa watu wote, lakini kwa mashahidi waliochaguliwa kabla na Mungu. - sisi wenyewe, tulio kula naye na kunywa naye baada ya kufufuka kutoka kwa wafu. 42 Ametuagiza kuhubiri kwa watu na kushuhudia kuwa huyu ndiye ambaye amechanguliwa na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na waliokufa. 43 Katika yeye manabii wote washuhudia, ili kwamba kila anayeamini katika yeye hupokea msamaha wa dhambi kupitia jina lake." 44 Wakati Petro akiendelea kusema haya, Roho Mtakatifu akawajaza wote waliokuwa wakisikiliza ujumbe wake. 45 Watu waliokuwa kwa kundi la tohara la waumini - wale wote waliokuja na Petro- walishangazwa, kwa sababu ya karama ya Roho Mtakatifu aliyemwagwa pia kwa watu wa mataifa. 46 Kwa kuwa walisikia hawa watu wa mataifa wakizungumza kwa lugha zingine na kumtukuza Mungu. Kisha Petro akajibu, 47 "Kuna mtu yeyote anaweza kuzuia maji ili watu wasibatizwe, Watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi?" 48 Ndipo akawaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Baadaye wakamwomba akae nao kwa siku kadhaa.