Sura 1 3

1 Ole kwa mji uliojaa damu! Wote umejaa uongo na mali za wizi; waadhiriwa wapo kwake daima. 2 Lakini sasa kuna kelele za mijeledi na sauti za magurudumu yanayozunguka, farasi wanaokimbia, na magari ya vita yanao rukaruka. 3 Wapanda farasi wanashambulia,panga zinameremeta na mikuki inang'aa, marundo ya maiti, idadi kubwa ya miili isiyohesabika-washambuliaji wanajikwaa juu yake. 4 Hii inatokea kwa sababu ya matendo ya tamaa ya kahaba mrembo, mtaalam wa uchawi, mwenye kuuza mataifa kupitia kwa ukahaba wake, na watu kupitia matendo yake ya kichawi. 5 " Tazama, mimi nipo kinyume na wewe --- hili ni neno la Yehova wa majeshi-- sketi yako nitaiinua juu ya uso wako na kuzionyesha sehemu zako za siri kwa mataifa, aibu yako kwa falme. 6 Nitarusha uchafu wa kuchukiza kwako na kukufanya uwe mbaya sana; nitakufanya uwe mtu wa kutazamwa na kila mmoja. 7 Itakuwa kwamba kila mmoja anayekutazama atakukimbia na kusema, 'Ninawi ameharibika; ni nani ataomboleza kwa ajili yake?' Ni wapi nitampata mtu anayeweza kukufariji?" 8 Ninawi, je wewe ni bora kuliko No-amoni, uliojengwa juu ya Mto Naili, uliokuwa umezungukwa na maji, ambao ulinzi wake ilikuwa bahari, na bahari ilikuwa ukuta wake? 9 Ethiopia na Misri walikuwa nguvu zake, na mwisho wake haukuwepo; Putu na Libya walikuwa rafiki zake. 10 Lakini No-amoni alichukuliwa; alikwenda kwenye mateka; watoto wake wadogo walivunjwa vipande vipande katika kila makao makuu ya mtaa; adui zake walipiga kura kwa watu wake wenye heshima, na wakuu wake wote walifungwa minyororo. 11 Wewe pia utalewa; utajaribu kujificha, na utatafuta kimbilio kutoka kwa adui yako. 12 Ngome zako zote zitakuwa kama mitini yenye tini zilizoiva mapema: kama zikitikiswa, zitaangukia ndani ya kinywa cha mlaji. 13 Tazama, watu miongoni mwenu ni wanawake; malango ya nchi yako yamefunguliwa wazi kwa adui zako; moto umeharibu bawaba zake. 14 Nenda ukachote maji kwa ajili ya kuzingirwa; ziimarishe ngome zako; nenda kwenye udongo na kandamiza matope; finyanga kwa ajili ya matofali. 15 Moto utakuteketeza pale, na upanga utakuangamiza. Utateketezwa kama nzige wachanga wanavyoteketeza kila kitu. Ninyi wenyewe mjitengeneze kuwa wengi kama nzige wachanga, na wengi kama nzinge waliopevuka. 16 Umezidisha wafanyabiashara wako zaidi kuliko nyota mbinguni; lakini wapo kama nzige wachanga;wanapora nchi na kisha kuruka kwenda zake. 17 Wafalme wenu wapo kama kundi la nzige, na wakuu wenu wa majeshi ni kama nzige watuao kwenye ukuta wakati wa siku ya baridi. Lakini jua linapowaka wanaruka kwenda zao; na mahali waendapo hakuna anayepajua. 18 Mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wamelala; watawala wako wamejilaza chini kupumzika. Watu wako wametawanyika juu ya milima, na hakuna hata mmoja wa kuwakusanya. 19 Hakuna uponyaji unaowezekana kwa ajili ya vidonda vyako. Vidonda vyako ni vikubwa. Kila anayesikia habari zako atapiga makofi kwa furaha juu yako. Ni nani ambaye hajaguswa na uovu wako wa daima?