Sura 1 2

1 Yule ambaye atakutawanya anakuja dhidi yako. Linda kuta za mji, linda barabara, imarisha viuno vyako, kusanya nguvu zako zote. 2 Maana Yehova anarejesha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli, ingawa wateka nyara waliwaharibu na kuharibu matawi ya zabibu zao. 3 Ngao za mashujaa wake ni nyekundu, na askari wamevaa nguo nyekundu; magari ya vita yanang'ara na vyuma vyake katika siku ambayo yaliandaliwa,na mikuki ya mivinje inarushwa hewani. 4 Magari ya vita yanapita kasi kwenye mitaa; yanakimbia nyuma na mbele kwenye mitaa mipana. Yapo kama mienge, na yanakimbia kama umeme. 5 Huwakumbuka mashujaa wake; wanajikwaa kila mmoja kwa mwingine katika kutembea kwao; wanaharakisha kuushambulia ukuta wa mji. Ngao kubwa imetayarishwa kuwakinga hawa washambuliaji. 6 Malango kwenye mito yamelazimishwa kufunguka, na jumba la mfalme limeanguka . 7 Huzabu amevuliwa mavazi yake na amachukuliwa; watumishi wake wa kike wanaomboleza kama njiwa, wakipiga vifua vyao. 8 Ninawi ni kama bwawa la maji linalovuja, huku watu wake wakikimbia kama maji yanayotiririka. Wengine wanasema, " Simama, simama," lakini hakuna anayegeuka nyuma. 9 Chukua nyara ya fedha, chukua nyara ya dhahabu, maana hakuna mwisho wa hazina , kwa fahari ya vitu vyote vizuri vya Ninawi. 10 Ninawi ipo tupu; tupu na imeharibiwa. Moyo wa kila mtu unayeyuka, magoti ya kila mmoja yanagongana pamoja, na uchungu upo kwa viuno vya kila mmoja; sura zao wote zimepauka. 11 Sasa liko wapi pango la simba, sehemu ambapo wana-simba wadogo hula chakula, sehemu ambapo simba dume na simba jike walitembea, na wana-simba, ambapo hawakuogopa kitu chochote? 12 Simba alirarua mawindo yake vipande vipande kwa ajili ya watoto wake; aliwanyonga mawindo wake kwa ajili ya wake zake, na kulijaza pango lake mawindo, tundu lake kwa mizoga iliyoraruliwa. 13 "Tazama, mimi nipo kinyume na wewe- hili ni neno la Yehova wa majeshi. Nitayachoma magari yenu ya vita katika moshi, na upanga utameza wana-simba wenu . Nitakatilia nyara zenu kutoka kwenye nchi yenu, na sauti za wajumbe wenu hazitasikika tena."