sura ya 2

1 Ndugu zangu katika Kristo msiifuate imani ya Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, kwa kupendelea watu fulani. 2 Kama mtu fulani akiingia kwenye mikutano yenu amevaa pete za dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia masikini mwenye mavazi machafu, 3 na mkaonyesha kumjali zaidi yule mwenye mavazi mazuri na kusema, "Tafadhari wewe keti hapa mahali pazuri" lakini mkamwambia yule masikini, "Wewe simama pale," au "Kaa chini ya miguu yangu." 4 Je, hamuhukumiani ninyi wenyewe, na kuwa waamuzi wenye mawazo mabaya? 5 Sikilizeni, ndugu zangu wapendwa, je, Mungu hakuwachagua watu masikini wa dunia hii kuwa matajiri katika imani na warithi ufalme wa Mungu aliowaahidia wampendao? 6 Lakini mmewadharau masikini! Je, watu matajiri wanaowatendea ninyi mabaya, sindio hao wanaowaburuta ninyi mahakamani? 7 Je, si matajiri wanaolitukana jina lile zuri la Yesu kristo ambalo kwalo mnaitiwa? 8 Hivyo, basi kama mwaitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa katika maandiko, "Utampenda kila mtu kama wewe mwenyewe unavyojipenda," mwafanya vyema. 9 Lakini kama mkipendelea baadhi ya watu, matajiri na wenye vyeo mnatenda dhambi, mwahukumiwa na sheria kuwa ni wavunja sheria. 10 Kwa kuwa yeyote anayetii sheria yote, na bado akajikwaa katika jambo moja tu, amekuwa na hatia ya kuvunja sheria yote! 11 Kwa kuwa Mungu aliyesema, "Usizini," ndiye pia aliyesema, "Usiue." Kama hauzini, lakini una uwa, umekwishavunja sheria za Mungu. 12 Kwa hiyo kile mnachoweza kukisema manapaswa kutii kama wale ambao Mungu atawahukumu kulingana na sheria inayotoa uhuru wa kweli. 13 Kwa kuwa hukumu huja pasipo huruma kwa wale wasio na huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu. 14 Kuna uzuri gani, ndugu zangu, kama mtu anasema ninayo imani kwa Mungu, lakini hana matendo mema? Je, imani hiyo yaweza kumwokoa mtu huyo kutoka kwenye hukumu ya mungu? 15 Kama ndugu wa kiume au wa kike ni muhitaji wa mavazi au chakula cha kila siku, 16 na mmoja wenu akawaambia, "Nendeni kwa amani, mkaote moto na mle vizuri," lakini hamuwapi mahitaji muhimu ya mwili, hiyo yafaaa nini? 17 Hali kadhalika, imani pekee, kama haina matendo mema, imekufa. 18 Lakini mtu fulani anaweza kushindana kusema, " Una imani, na mimi ninayo matendo." Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu. 19 Ndugu zangu kwakuwa tunaamini kuna Mungu mmoja; tuko sahihi. Hata mapepo nayo yanaamini hivyo na kutetemeka. 20 Je, unataka kujua, ewe mtu mpumbavu, namna ambavyo imani hiyo pasipo matendo mema isivyofaa? 21 Je, Abrahamu baba yetu alihesabiwa haki kwa matendo alipomtoa mwanawe Isaka juu ya madhabahu? 22 Mnaona jinsi imani yake ilifanya kazi na matendo yake mema, na kwa matendo yake, imani yake ilifikia kusudio lake. 23 Maandiko yalitimizwa yasemayo, "Abrahamu alimwamini Mungu, na akahesabiwa kuwa ni mwenye haki." Hivyo Abrahamu aliitwa rafiki wa Mungu. 24 Mwaona kuwa kwa matendo mtu huhesabiwa haki, na si kwa imani tu. 25 Hali kadhalika, Rahabu yule kahaba, je! alihesabiwa haki kwa matendo, alipowakaribisha wajumbe na kuwapeleka kwa barabara nyingine? 26 Kwa kuwa kama vile mwili usipokuwa na roho umekufa, vivyo hivyo imani pasipo matendo imekufa.