sura ya 1

1 Mimi Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, kwa makabila kumi na mbili yaliyotawanyika, nawasalim. 2 Hesabuni kuwa ni furaha zaidi, ndugu zangu, mnapopita katika majaribu mbali mbali, 3 mkijua kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huwapa uvumilivu. 4 Basi acheni uvumilivu uikamilishe kazi yake, ili kwamba muweze kukomaa kikamilifu, bila kupungukiwa neno lolote. 5 Lakini kama mtu kati yenu anahitaji hekima, aiombe kutoka kwa Mungu, ambaye hutoa kwa ukarimu na pasipo kukemea kwa wote wamwombao, Mungu atawapa hekima. 6 Lakini aombe kwa imani, bila shaka, kwa kuwa mwenye mashaka ni kama mawimbi katikati ya bahari, huchukuliwa na upepo na kutupwa huku na huko. 7 Kwa hakika mtu huyu asifikirie kwamba atapokelewa ombi lake kutoka kwa Bwana; 8 mtu huyu ana nia mbili, hana msimamo katika njia zake zote. 9 Lakini ndugu aliye maskini anapaswa kujivuna katika kusimama kwake juu na ame kutukuzwa, 10 wakati huo huo ndugu aliye tajiri awe na unyenyekevu wake, kwa sababu atatoweka kama ua la kondeni katika shamba. 11 Jua huchomoza na joto huukunguza na kukausha mimea, na maua huanguka na uzuri wake hupotea. Vivyo hivyo watu matajiri watachakaa katikati ya kazi zao. 12 Amebarikiwa mtu yule anayevumilia majaribu, kwa kuwa baada ya kushinda jaribu hilo, atapokea taji ya uzima, ambayo imeahidiwa kwa wale wampendao Mungu. 13 Mtu yeyote hapaswi kusema anapojaribiwa, "Kwamba jaribu hili latoka kwa Mungu," kwa sababu Mungu hajaribiwi na mambo mauovu, na Mungu mwenyewe hamjaribu mtu yeyote. 14 Bali kila mtu hujaribiwa na tamaa zake mbaya za mambo maovu zinazomshawishi na kumvuta kwenda mbali na Mungu. 15 Ndipo baada ya tamaa ya dhambi kubeba mimba, ya dhambi huzaliwa, dhambi ikiisha kukomaa sawasawa, huzaa mauti. 16 Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike. 17 Kila zawadi iliyo nzuri na kila zawadi iliyokamilika hutoka juu, hushuka chini kutoka kwa Baba wa nuru. Yeye habadilika kama kivuli kibadilikavyo. 18 Mungu alichagua kutupa sisi uzima kwa Neno la kweli, ili kwamba tuweze kuwa kama uzao wa kwanza miongoni mwa viumbe vyake. 19 Mnajua hili, ndugu zangu wapendwa. Kila mmoja anapaswa kuwa mwepesi wa kusikiliza, siyo mwepesi wa kuongea wala kukasirika, 20 kwa kuwa hasira ya mwanadamu haiwezi kutenda haki ya Mungu. 21 Kwa hiyo wekeni mbali uchafu wa dhambi na ubaya wote ulio mahali popote, na kwa unyenyekevu lipokeeni neno lililopandwa ndani yenu, ambalo lina uwezo wa kuokoa roho zenu kutoka kwenye hukumu ya Mungu. 22 Lakini litiini lile neno, msiishie kulisikiliza tu, mnajidanganya nafsi zenu wenyewe. 23 Kwa kuwa kama yeyote alisikiaye neno bila kulitendea kazi ni sawa na mtu ajiangaliaye uso wake kwenye kioo kama ulivyo. 24 Hujitathimini uso wake, na huenda zake na baada ya muda mfupi husahau anavyofanana. 25 Bali mtu yule anayeiangalia kwa uangalifu sheria kamili, sheria ya uhuru, na kuendelea kuitii, si kwa sababu yeye ni msikilizaji tu anayesahau, Mungu atambariki mtu anapoitenda neno. 26 Ikiwa mtu yeyote atafikiri mwenyewe moyoni mwake kuwa ni mtu wa dini, lakini hawezi kuudhibiti ulimi wake, ajidanganya moyo wake anamwabudu Mungu bure. 27 Dini iliyo safi na isikataliwa mbele za Mungu wetu na Baba wa mbinguni ni hii: kuwasaidia yatima na wajane katika mateso yao, na kujilinda mwenyewe na ufisadi wa dunia.