Sura 17

1 Sasa walipokuwa wamepitia katika miji ya Amfipoli na Apolonia, walikuja mpaka mji wa Thesalonike ambao kulikuwa na sinagogi la Wayahudi. 2 Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake , alienda kwao, na kwa muda wa siku tatu za Sabato alijadiliana nao juu ya maandiko. 3 Alikuwa akiwafungulia maandiko na kuwaeleza kuwa, ilimpasa Kristo ateseke na kisha kufufuka tena kutoka kwa wafu. Alisema, "Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Kristo" 4 Baadhi ya Wayahudi walishawishika na kuungana na Paulo na Sila, pamoja na idadi kubwa ya Wayunani wacha Mungu, na sio wanawake wachache walioongoza. 5 Lakini baadhi ya Wayahudi wasioamini, waliojawa na wivu, walienda sokoni na kuwachukuwa baadhi ya watu waovu, wakakusanya umati wa watu pamoja, na kusababisha ghasia mjini, kisha wakaivamia nyumba ya Jason, wakitaka kuwakamata Paulo na Sila ili kuwaleta mbele za watu. 6 Lakini walipowakosa, walimkamata Yasoni na baadhi ya ndugu wengine na kuwapeleka mbele ya maofisa wa mji, wakipiga kelele, " Hawa wanaume walioupindua ulimwengu wamefika mpaka huku pia, 7 Wanaume hawa waliokaribishwa na Yasoni wanaihalifu sheria ya Kaisari, wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu" 8 Umati na maofisa wa mji waliposikia mambo hayo, waliingiwa na wasiwasi. 9 Baada ya kuwa wamekwisha kuchukua fedha ya thamani ya ulinzi kutoka kwa Yason na wengine, waliwaachia waende. 10 Usiku ule ndugu walimtuma Paulo na Sila Beroya. Na walipofika kule walikwenda katika sinagogi la Wayahudi. 11 Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale watu wa Thesalonike, kwa sababu walikuwa na utayari wa kulipokea neno kwa akili zao, na kuchunguza maandiko kila siku ili kuona kama maneno yaliyonenwa ndivyo yalivyo. 12 Kwa hiyo wengi wao waliamini, wakiwemo wanawake wenye ushawishi mkubwa wa Kiyunani na wanaume wengi. 13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo pia alikuwa akitangaza neno la Mungu huko Beroya, walienda huko na kuchochea na kisha kuanzisha ghasia kwa watu. 14 Basi mara moja, ndugu walimpeleka Paulo kwa njia ya ziwa, lakini Sila na Timotheo wakabaki pale. 15 Wale ndugu waliokuwa wakimuongoza Paulo walienda naye hadi Athene, walipomwacha Paulo huko, walipokea maagizo kutoka kwake kuwa, Sila na Timotheo waje kwake kwa haraka iwezekanavyo. 16 Na wakati akiwasubiri huko Athene, roho yake ilikasirishwa ndani yake kwa jinsi alivyouona mji ulivyojaa sanamu nyingi. 17 Hivyo akajadiliana katika sinagogi na wayahudi wale waliomcha Mungu na kwa wale wote aliokutana nao kila siku sokoni. 18 Lakini baathi ya Waepikureo na Wastoiko, wenye ujuzi wakakutana naye. Na wengine wakasema, " Ni nini anachokisema huyu mpiga porojo? Wengine wakasema, "anaonekana ni mtu anayetangaza habari za miungu migeni," kwa sababu anahubiri habari ya Yesu na ufufuo. 19 Wakamchukua Paulo na kumleta Areopago, wakisema, "Twaweza kujua haya mafundisho mapya unayoyaongea? 20 Kwani unaleta mambo mapya katika masikio yetu. Kwahivyo tunataka kujua haya mambo yana maana gani?" 21 (Na watu wote wa Athene pamoja na wageni waliopo kwao, walitumia muda wao aidha katika kuongea na kusikiliza juu ya jambo jipya.) 22 Kwa hiyo Paulo akasimama katikati ya watu wa Areopago na kusema, "Enyi watu wa Athene, naona kuwa ninyi ni watu wa dini kwa kila namna, 23 Kwani katika kupita kwangu na kuangalia vitu vyenu vya kuabudu, nimeona maneno yalioandikwa kwenye moja ya madhabahu yenu, ikisema "KWA MUNGU ASIYEJULIKANA". Hivyo basi, huyo mnayemwabudu pasipokujua, ndiye ninayewajulisha ninyi. 24 Mungu aliyeumba dunia na kila kitu kilichoko ndani yake, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hawezi kukaa katika mahekalu yaliyotengenezwa na mikono. 25 Na pia hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu kwao, kwani yeye mwenyewe huwapa watu uzima na pumzi na vitu vingine vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, alifanya mataifa yote ya watu waishio juu ya uso wa dunia, baada ya kuamua majira na mipaka yao iliyowekwa katika maeneo walioishi, 27 ili wamtafute Mungu, na yamkini wamfikie na kumpata. Na kwa uhakika hayupo mbali na kila mmoja wetu. 28 Kwani ndani yake tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu, kama vile mtunzi wenu mmoja wa shairi aliposema 'tu wazaliwa wake.' 29 Kwa hiyo, ikiwa sisi ni wazaliwa wa Mungu, hatupaswi kufikiri kuwa sifa za uungu ni kama dhahabu, au shaba, au mawe, sanamu iliyochongwa kwa ustadi na mawazo ya watu. 30 Kwa hiyo, Mungu alijifanyakutojali nyakati zile za ujinga, lakini sasa anaamuru watu wote kila mahali wapate kutubu. 31 Hii ni kwa sababu ameweka siku atakayo ihukumu dunia kwa haki kwa mtu ambaye aliyemchagua. Mungu ametoa ushahidi wa mtu huyu kwa kila mtu pale alipomfufua katoka kwa wafu." 32 Sasa watu wa Athene waliposikia habari ya kufufuliwa kwa wafu, baadhi yao walimdhihaki Paulo, ila wengine wakasema "Tutakusikiliza tena kwa habari ya jambo hili" 33 Baada ya hapo, Paulo akawaacha. 34 Lakini baadhi ya watu waliungana naye wakaamini, akiwemo Dionisio Mwareopago, Mwanamke anaitwa Damari na wengine pamoja nao.