Sura 1

1 Kitabu cha zamani nilikiandika, Theofilo, nikisema yote Yesu aliyoanza kufanya na kufundisha, 2 mpaka siku ambayo Yeye alipokelewa juu. Baada ya kutoa amri kupitia Roho Mtakatifu kwa mitume aliokuwa amewachagua. 3 Baada ya mateso yake, Yeye alijiwasilisha kwao akiwa hai pia na vithibitisho vingi vikishuhudia. Kwa siku arobaini alijiweka wazi kwao, na alizungumza kuhusu ufalme wa Mungu. 5 4 Alipokuwa akikutana pamoja nao, aliwaamuru wasiondoke Yerusalemu, lakini wasubiri kwa ajili ya ahadi ya Baba, ambayo alisema, "Mlisikia kutoka kwangu kwamba Yohana alibatiza kabisa kwa maji lakini mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu kwa siku chache." 6 Na walipokuwa wamekutanika pamoja walimuuliza, "Bwana, je, huu ndio muda utakaowarudishia Israeli ufalme?" 7 Yeye akawaambia, "Siyo sawa kwenu kujua wakati au majira ambayo Baba amekusudia kwa mamlaka yake mwenyewe." 8 Lakini mtapokea nguvu, wakati Roho Mtakatifu atakapokuja juu yenu, na ninyi mtakuwa mashahidi wangu kote katika Yerusalemu na Yudea yote na Samaria mpaka mwisho wa dunia." 9 Bwana Yesu alipokwisha kuwa ameyasema haya, wakiwa wanatazama juu, Yeye aliinuliwa juu, na wingu likamkinga wasimwone kwa macho yao. 10 Wakati wanatazama mbinguni kwa makini akienda, ghafla, watu wawili walisimama katikati yao wamevaa mavazi meupe. 11 Walisema, "Enyi watu wa Galilaya, kwa nini mnasimama hapa mkitazama mbinguni?" Huyu Yesu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu akapaa juu mbinguni atarudi kwa namna ile ile kama mlivyomuona akienda mbinguni. 12 Ndipo wakarudi Yerusalemu kutoka kwenye mlima ambao unaitwa wa mizeituni, ambao uko karibu na Yerusalemu, kiasi cha umbali wa kutembea mwendo wa Sabato. 13 Walipofika walikwenda ghorofani walikokuwa wakikaa. Nao ni Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Thomaso, Batholomayo, Mathayo, Yakobo Mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda Mwana wa Yakobo. 14 Wote walikuwa wamejitolea kwa nia moja kuomba, miongoni mwao walikuwemo wanawake, na Mariamu Mama yake Yesu, na kaka zake. 15 Katika siku zile Petro alisimama katikati ya hao ndugu, kama watu 120, akasema, 16 Ndugu, ilikuwa lazima kwamba maandiko yatimizwe, ambapo zamani Roho Mtakatifu alisema kwa kinywa cha Daudi kuhusiana na Yuda, ambaye aliwaelekeza wale waliomkamata Yesu. 17 Kwa kuwa yeye alikuwa mmoja wetu na alipokea fungu lake la faida katika huduma hii." 18 (Sasa mtu huyu alinunua eneo kwa kile alichokipokea kwa uovu wake na hapo alianguka akitanguliza kichwa, mwili ukapasuka na matumbo yake yote wazi yakamwagika. 19 Wote walioishi Yerusalemu walisikia kuhusu hili, hivyo eneo hilo wakaliita kwa lugha yao "Akeldama," kwamba ni "Shamba la Damu.") 20 "Kwenye kitabu cha Zaburi imeandikwa, 'Ngoja eneo lake lifanwe kuwa mahame na asiruhusiwe hata mtu mmoja kuishi pale;' 'Acha mtu mwingine achukue nafasi yake ya uongozi.' 21 Ni muhimu, kwa hiyo, kwamba mmoja wa wanaume ambao waliambatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipotoka na kuingia kati yetu, 22 kuanzia kwenye ubatizo wa Yohana mpaka siku ile alipotwaliwa juu, awe shahidi wa ufufuo pamoja nasi. 23 "Wakaweka mbele wanaume wawili, Yusufu aitwaye Barsaba, ambaye pia aliitwa Yusto, na Mathia. 24 Wao waliomba wakisema, "Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, hivyo weka wazi yupi kati ya wawili hawa ambaye umemchagua 25 kuchukua nafasi katika huduma na utume, ambapo Yuda alitenda uovu na kwenda mahali pake." 26 Wakapiga kura kwa ajili yao, na kura ikamwangukia Mathia ambaye alihesabiwa pamoja na wale mitume kumi na moja.