Sura 9

1 Akawaambia, "Amin nawaambia, wako baadhi yenu wasimamao hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu." 2 Na baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana pamoja naye juu ya mlima, peke yao. Kisha akageuka sura mbele yao. 3 Mavazi yake yakang'aa sana, meupe sana, meupe zaidi kuliko mng'arishaji yoyote duniani angeweza kuyafanya kuwa meupe. 4 Kisha Eliya pamoja na Musa walitokea mbele yao, na walikuwa wakiongea na Yesu. 5 Petro alijibu akamwambia Yesu, "Mwalimu, ni vyema sisi kuwa hapa, na tujenge vibanda vitatu, kimoja kwa ajili yako, kimoja kwa ajili Musa na kingine kwa ajili ya Eliya." 6 (Kwa maana hakujua la kusema maana waliogopa sana.) 7 Wingu likaja na kuwafunika. Kisha sauti ikatoka katika lile winguni, " Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikieni yeye." 8 Ghafla, walipotazama huku na huko, hawakumuona tena mtu yeyote pamoja nao, isipokuwa Yesu tu. 9 Walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, akawaamuru wasimwambia mtu yeyote yale yote waliyoyaona, mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuka kutoka kwa wafu. 10 Kwa hiyo wakaweka jambo hilo ndani yao wenyewe, lakini walijadiliana wao kwa wao ni nini maana yake "kufufuka kutoka kwa wafu" 11 Walimwuliza Yesu,"Kwa nini waandishi husema lazima Eliya aje kwanza?" 12 Akawaambia, "Eliya anakuja kwanza kurejesha mambo yote. Kwa nini basi imeandikwa kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kudharauliwa? 13 Lakini nawaambia ya kwamba Eliya amekuja, na wakamfanyia walivyotaka, kama ilivyoandikwa juu yake. 14 Na walipofika kwa wanafunzi, waliona kundi kubwa limewazunguka na waandishi walikuwa wanabishana nao. 15 Na mara walipomwona Yesu, kundi lote lilishangaa na kumkimbilia kumsalimia. 16 Aliwauliza wanafunzi wake, "Mnabishana nao juu ya nini?" 17 Mtu mmoja katika kundi alimjibu, "Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako; ana roho inayomfanya asiweze kuongea, 18 humkamata na kumwangusha chini, naye anatoa povu mdomoni na kusaga meno na kuwa mgumu. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo, lakini hawakuweza. 19 Akawajibu, "Kizazi kisichoamini, nitakaa nanyi hadi lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu." 20 Wakamleta yule mvulana kwake. Roho mchafu alipomwona Yesu, ghafla ilimtia katika kutetemeka. Mvulana alianguka chini na kutoa povu mdomoni. 21 Yesu alimwuliza baba yake, "Amekuwa katika hali hii kwa muda gani?" Baba alisema, " Tangu utoto. 22 Mara nyingine humwangusha katika moto au kwenye maji, na kujaribu kumwangamiza. Kama unaweza kufanya chochote tuhurumie na utusaidie." 23 Yesu akamwambia, "'Kama unaweza'? Kila kitu kinawezekana kwa yeyote aaminiye." 24 Ghafla baba wa mtoto alilia na kusema, " Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu." 25 Wakati Yesu alipoona kundi linawakimbilia, alimkemea roho mchafu na kusema, "wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru toka kwake, usimwiiingie tena." 26 Ikalia na kumhangaisha mvulana kwa nguvu na kisha ikamtoka. Mvulana alionekana kama amekufa, Ndipo wengi wakasema, "Amekufa," 27 Lakini Yesu alimchukua kwa mkono akamwinua, na mvukana akasimama. 28 Wakati Yesu alipoingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, "Kwa nini hatukuweza kuitoa?" 29 Akawaambia, " Aina hii hatoki isipokuwa kwa maombi." 30 Wakatoka pale na kupitia Galilaya. Hakutaka mtu yeyote ajue walipo, 31 kwa kuwa alikuwa anafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, "Mwana wa Adamu atapeanwa mikononi mwa watu, na watamuua. Atakapokuwa amekufa, baada ya siku tatu atafufuka tena." 32 Lakini hawakuelewa maelezo haya, na waliogopa kumwuliza. 33 Ndipo walifika Karperinaumu. Baada ya kuingia ndani ya nyumba akawauliza, ''Mlikuwa mnajadili nini njiani"? 34 Lakini walikuwa kimya. Kwani walikuwa wanabishana njiani kwamba nani alikuwa mkubwa zaidi. 35 Alipoketi chini akawaita kumi na wawili pamoja, na akawambia, "Kama yeyote anataka kuwa wa kwanza, ni lazima awe wa mwisho na mtumishi wa wote." 36 Akamchukua mtoto mdogo akamweka katikati yao. Akamchukua katika mikono yake na akawambia, 37 "Yeyote ampokeaye mtoto kama huyu kwa jina langu, pia amenipokea mimi, na ikiwa mtu amenipokea, hanipokei mimi tu, lakini pia aliyenituma." 38 Yohana akamwambia, "Mwalimu, tulimwona mtu anatoa pepo kwa jina lako na tukamzuia, kwa sababu hatufuati." 39 Lakini Yesu akasema, "Msimzuie, kwa kuwa hakuna atakayefanya kazi kubwa kwa jina langu na kisha baadaye aseme neno baya lolote juu yangu. 40 Yeyote asiyekuwa kinyume nasi yuko upande wetu. 41 Yeyote atakayekupa kikombe cha maji ya kunywa kwa sababu wewe niwa Kristo, Amin nawaambia, hatapoteza thawabu yake. 42 Yeyote anayewakosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio mimi, ingekuwa vyema kwake kufungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutupwa baharini. 43 Kama mkono wako ukikukosesha ukate. Ni heri kuingia katika uzima bila mkono kuliko kuingia kwenye kuzimu ukiwa na mikono yote, katika moto usiozimika. 44 (Zingatia: Mstari hii, "Mahali ambapo funza hawafi na moto usiozimika." haumo katika nakala za kale). 45 Kama mguu wako ukikukosesha, ukate. Ni vyema kwako kuingia uzimani ukiwa kilema, kuliko kutupwa kuzimu na miguu miwili. 46 (Zingatia: Mstari huu, "Mahali ambapo funza hawafi na moto usioweza kuzimika" haumo kwenye nakala za kale). 47 Kama jicho lako likikukosesha ling'oe. Ni vyema kwako kuingia katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili na kutupwa kuzimu. 48 Mahali ambapo funza wao hawafi, na moto usiozimika. 49 Kwa maana kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. 50 Chumvi ni nzuri, lakini kama chumvi ikipoteza ladha yake, unawezaje kuifanya iwe chumvi tena? Muwe na chumvi ninyi kwa ninyi na muwe na amani mmoja na mwingine."