Sura 16

1 Wakati sabato ilipokwisha, Mariamu Magdalena na Mariamu mama yake na Yakobo, na Salome, walinunua manukato mazuri, ili waweze kuja na kuupaka mafuta mwili wa Yesu. 2 Asubuhi na mapema siku ya kwanza ya juma, walienda kwenye kaburi wakati jua lilipochomoza. 3 Wakisemezana wao kwa wao, "Nani ataliviringisha jiwe kwa ajili yetu ili tuingie kaburini?" 4 Wakati walipotazama, waliona ya kuwa jiwe limekwisha kuvingirishwa jiwe, nalo lilikuwa kubwa sana. 5 Wakaingia kwenye kaburi na wakamwona kijana amevaa joho jeupe, ameketi upande wa kulia, na wakashangazwa. 6 Akawaambia, "Msiogope. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulibiwa. Amefufuka! Hayupo hapa. Tazama mahali pale walipokuwa wamemweka. 7 Lakini nendeni, mkawaambie wanafunzi wake na Petro ya kuwa amewatangulia kuelekea Galilaya. Huko mtamwona, kama alivyokua amewaambia." 8 Wakaondoka na kukimbia kutoka kwenye kaburi; wakitetemeka na kushangaa. Hawakusema chochote kwa mtu yeyote sababu waliogopa sana. 9 (Zingatia: Nakala za kale hazina Marko 16: 9-20) Mapema katika siku ya kwanza ya juma, baada ya kufufuka, alimtokea kwanza Mariamu Magdalena, ambaye kutoka kwake alimtoa mapepo saba. 10 Aliondoka na kuwaambia wale ambao walikuwa pamoja naye, wakati walipokuwa wakiomboleza na kulia. 11 Wakasikia kwamba yu hai na ameonekana naye, lakini hawakumwamini. 12 (Zingatia: Nakala za kale hazina Marko 16: 9-20) Baada ya mambo haya, alionekana katika sura tofauti na wawili wao walipokuwa wakienda mashambani. 13 Wakarudi na kuwaambia wanafunzi wengine waliobaki, lakini hawakuwaamini. 14 (Zingatia: Nakala za kale hazina Marko 16: 9-20) Yesu baadaye akajitokeza kwa wale kumi na mmoja walipokuwa wakiegemea mezani, na akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo, kwa sababu hawakuwaamini wale waliomwona baada ya kufufuka kutoka kwa wafu. 15 Akawaambia, " Enendeni ulimwenguni mwote, na kuhubiri injili kwa viumbe vyote. 16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokolewa, na yule asiyeamini atahukumiwa. 17 (Zingatia: Nakala za kale hazina Marko 16: 9-20) Ishara hizi zitaambatana na wote waaminio. Kwa jina langu watatoa pepo. Watasema kwa lugha mpya. 18 Watashika nyoka kwa mikono yao, na hata wakinywa kitu chochote cha kufisha hakitawadhuru. Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya". 19 Baada ya Bwana Yesu kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu. 20 Wanafunzi wakaondoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akitenda kazi pamoja nao na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizoambatana nao.