Sura 14

1 Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya Mikate isiyotiwa Chachu. Makuhani wakuu na waandishi walikuwa wakitafuta namna ya kumkamata Yesu kwa siri na kumuua. 2 Maana walikua wanasema, "Sio wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia." 3 Wakati Yesu alipokuwa Bethania nyumbani kwa Simoni mkoma, na alipokuwa akiegemea mezani, mwanamke mmoja akakuja kwake akiwa na chupa ya alabasta yenye manukato ya thamani kubwa, ambayo ni nardo safi. Akaivunja ile chupa na kumwaga ile nardo kichwani mwake. 4 Lakini kulikuwa na baadhi yao waliokasirika. Wakazungumza wao kwa wao na kusema, "Ni nini sababu ya upotevu wa manukato haya? 5 Manukato haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari mia tatu, na wakapewa maskini." Kisha wakamkemea. 6 Lakini Yesu akasema, "Mwacheni. Kwa nini mnamsumbua? Amefanya jambo zuri kwangu. 7 Siku zote mnao maskini pamoja nanyi, na wakati wowote mnapotamani mnaweza kufanya mazuri kwao, lakini hamtakuwa nami wakati wote. 8 Amefanya kile anachoweza: ameupaka mwili wangu mafuta kwa ajili ya maziko. 9 Kweli nawaambia, kila mahali injili inapohubiriwa katika ulimwengu wote, kile alichofanya mwanamke huyu kitazungumzwa kwa ukumbusho wake. 10 Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale kumi na wawili, alikwenda kwa makuhani wakuu ili kwamba apate kumkabidhi kwao. 11 Wakati makuhani wakuu walisikia hivyo, walifurahi na wakaahidi kumpa fedha. Alianza kutafuta nafasi ya kumkabidhi kwao. 12 Siku ya kwanza ya mkate usiotiwa chachu, wakati walipotoa mwanakondoo wa pasaka, wanafunzi wake walimwambia, "Unataka twende wapi tukaandae ili upate kula mlo wa Pasaka?" 13 Akawatuma wawili wa wanafuzi wake na kuwaambia, "Nendeni mjini, na mwanamume amebeba mtungi wa maji atakutana nanyi. Mfuateni. 14 Nyumba atakayoingia, mfuateni na mmwambie mwenye nyumba hiyo, 'Mwalimu asema, "Kiko wapi chumba cha wageni mahali nitakapokula Pasaka na wanafunzi wangu?" 15 Atawaonesha chumba kikubwa cha juu kilicho na samani ambacho kiko tayari. Fanyeni maandalizi kwa ajili yetu pale." 16 Wanafunzi waliondoka wakaenda mjini. Walikuta kila kitu kama alivyokuwa amewaambia, na wakaandaa mlo wa Pasaka. 17 Wakati ilipokuwa jioni, alikuja na wale Kumi na wawili. 18 Na walipokuwa wakiikaribia meza na kula, Yesu alisema, "Kweli nawaambia, mmoja kati yenu anayekula pamoja nami atanisaliti." 19 Wote walisikitika, na mmoja baada ya mwingine walimwambia, "Hakika siyo mimi?" 20 Yesu alijibu na kuwaambia, "Ni mmoja wa Kumi na wawili kati yenu, mmoja ambaye sasa anachovya tonge katika bakuli pamoja nami. 21 Kwa kuwa Mwana wa Adamu atakwenda kama vile maandiko yasemavyo juu yake. Lakini ole wake mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu atasalitiwa! Ingekuwa vizuri zaidi kwake kama mtu yule asingezaliwa." 22 Na walipokuwa wakila, Yesu akachukua mkate, akaubariki, na kuumega. Aliwapa akisema, "Chukueni. Huu ni mwili wangu." 23 Akachukua kikombe, akashukuru, na akawapatia, na wote wakakinywea. 24 Akawaambia, "Hii ni damu yangu ya agano, damu imwagikayo kwa ajili ya wengi. 25 Kweli nawaambia, sitakunywa tena katika zao hili la mzabibu mpaka siku ile nitakapokunywa mpya katika ufalme wa Mungu." 26 Walipokwisha kuimba wimbo, walikwenda nje katika Mlima wa Mizeituni. 27 Yesu akawaaambia, "Ninyi nyote mtajitenga mbali nami, kwa kuwa imeandikwa, 'Nitampiga mchungaji na kondoo watatawanyika.' 28 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia mbele yenu Galilaya." 29 Petro alimwambia, "Hata kama wote watakuacha, mimi sitakuacha." 30 Yesu akamwambia, "Kweli nakuambia, leo-naam,usiku huu huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utakuwa umenikana mara tatu." 31 Lakini Petro akasema kwa msisitizo, "ikiwa ni lazima nife nawe, sitakukana." Wote walitoa ahadi ile ile. 32 Wakafika mahali paitwapo Gethsemane, na Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kaeni hapa wakati nasali." 33 Akawachukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye, akaanza kuhuzunika na kutaabika sana. 34 Aliwaambia, "Nafsi yangu ina huzuni sana, mpaka hatua kifo. Bakini hapa na mkeshe." 35 Yesu akaenda mbele kidogo, akaanguka chini, akaomba, kama ingewezekana, kwamba saa hii ingemwepuka. 36 Alisema, "Aba, Baba, Mambo yote yanawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini siyo mapenzi yangu, bali mapenzi yako." 37 Akarudi na kuwakuta wamelala, na akamwambia Petro, "Simoni, je umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja? 38 Kesheni na muombe kwamba msije mkaingia katika majaribu. Hakika roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu." 39 Akaenda tena na kuomba, na alitumia maneno yaleyale. 40 Aliporudi tena, akawakuta wamelala, kwa kuwa macho yao yalikuwa mazito. Hawakujua nini cha kumwambia. 41 Akarudi mara ya tatu na kuwaambia, "Bado mmelala na kupumzika? Yatosha! Saa imefika. Tazama! Mwana wa Adamu anasalitiwa mikononi mwa wenye dhambi. 42 Amkeni, twendeni. Tazama, yule anayenisaliti yuko karibu." 43 Alipokuwa bado anaongea, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili akafika, na kundi kubwa pamoja naye wenye mapanga na marungu, kutoka kwa makuhani wakuu, waandishi na wazee. 44 Wakati huo msaliti wake alikuwa amewapa ishara, akisema, Yule nitakayembusu, ndiye. Mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi." 45 Wakati Yuda alipofika, moja kwa moja alienda kwa Yesu na kusema, "Mwalimu!" Na akambusu. 46 Kisha wakamwekea mikono na kumkamata. 47 Lakini mmoja kati yao aliyesimama karibu naye akachomoa upanga wake akampiga mtumishi wa kuhani mkuu na kumkata sikio. 48 Yesu akawaambia, "Mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kama mnyang'anyi? 49 Wakati kila siku nilikuwa nanyi na nikifundisha hekaluni, hamkunikamata. Lakini hili limefanyika ili maandiko yatimie. 50 Na wale wote waliokuwa na Yesu walimwacha na kukimbia. 51 Kijana mmoja aliyekuwa amevaa vazi la kitani pekee alilokuwa amejizungushia, alikua anafuata Yesu. Wale watu walipomkamata , 52 aliiacha ile nguo ya kitani kukimbia uchi. 53 Walimwongoza Yesu kwa kuhani mkuu. Pale walikusanyika pamoja naye wakuu wa makuhani wote, wazee, na waandishi. 54 Sasa Petro akamfuata kwa mbali, kuelekea kwenye ua wa kuhani mkuu. Aliketi pamoja na maafisa, akiota moto ili kupata joto. 55 Wakati huo makuhani wakuu wote na Baraza zima la wayahudi walikuwa wakitafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumwua. Lakini hawakuupata. 56 Kwa kuwa watu wengi walileta ushuhuda wa uongo dhidi yake, lakini hata ushahidi wao haukufanana. 57 Baadhi walisimama na kuleta ushahidi wa uongo dhidi yake; wakisema, 58 "Tulimsikia akisema, 'Nitaliharibu hekalu hili lililotengenezwa kwa mikono, na ndani ya siku tatu nitajenga lingine lisilotengenezwa kwa mikono.'" 59 Lakini hata ushahidi wao haukufanana. 60 Kuhani mkuu akasimama katikati yao na akamwuliza Yesu, "Je, huna jibu? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?" 61 Lakini alikaa kimya na hakujibu chochote. Mara tena Kuhani mkuu akamhoji na kusema, "Je wewe ni Kristo, mwana wa Mbarikiwa?" 62 Yesu alisema, "Mimi ndiye. Na utamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kulia wa nguvu na akija na mawingu ya mbinguni." 63 Kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, "Je, bado tunahitaji mashahidi? 64 Mmesikia kufuru. Uamuzi wenu ni upi?" Na wote walimhukumu kama mmoja aliyestahili kifo. 65 Baadhi wakaanza kumtemea mate na kumfunika uso na kumpiga kwa ngumi zao na kumwambia, "Tabiri!" Maafisa walimchukua na kumpiga. 66 Huku Petro alipokuwa yuko chini uani, mtumishi mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu akaja kwake. 67 Alimwona Petro alipokuwa amesimama akiota moto, na akamtazama kwa karibu na kusema, , "Nawe pia ulikuwa na Mnazareti, Yesu". 68 Lakini alikanusha, akisema, "Sijui wala sielewi unachoongea!" Kisha akatoka ampaka langonii. Na jogoo akawika. (Zingatia; Mstari huu, "Na jogoo akawika" haumo kwenye nakala za kale). 69 Lakini mtumishi wa kike alimwona na alianza kuwaambia tena wale ambao walikuwa wamesimama pale, "Mtu huyu ni mmoja wao!" 70 Lakini alikana tena. Baadaye kidogo wale waliokuwa wamesimama pale walikuwa wakimwambia Petro, "Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya." 71 Lakini alianza kujiweka mwenyewe chini ya laana na kuapa, "Simjui huyu mtu mnayemzungumzia." 72 Mara jogoo aliwika mara ya pili. Kisha Petro akakumbuka maneno ambayo Yesu aliyokuwa amemwambia: "Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu." Na aliangua kilio.