Sura 13

1 Yesu alipokuwa akitembea kutoka hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake akamwuliza, "Mwalimu, tazama mawe haya na majengo yakushangaza!" 2 Yesu akamwambia, "Unaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalo salia juu ya jingine ambalo halitaangushwa chini". 3 Na alipokuwa amekaa juu ya Mlima wa Mizeituni kinyume na hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamwuliza kwa siri, 4 "Tuambie, mambo haya yatatokea lini? Ni nini dalili ya mambo haya kutokea?" 5 Yesu akaanza kuwaambia, "Kjihadharini mtu asiwapotoshe. 6 Wengi watakuja kwa jina langu wakisema, 'Mimi ndiye', na watawapotosha wengi. 7 Mtakaposikia habari za vita na fununu za vita, msiogope; mambo haya lazima yatokea, lakini mwisho bado. 8 Kwa maana taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme dhidi ya ufalme. Patakuwa na matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali, na njaa. Hayo ni mwanzo wa utungu. 9 Iweni macho. Watawapeleka hadi mabarazani, na mtapigwa katika masunagogi. Mtasimamishwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kama ushuhuda kwao. 10 Lakini injili lazima kwanza ihubiriwe kwa mataifa yote. 11 Watakapo wakamata na kuwakabidhi, msiogope kuhusu kile mtakachosema. Kwa maana katika saa huyo, mtapewa kile mtakachosema; haitakuwa nyinyi mnayesema, bali Roho Mtakatifu. 12 Ndugu atamsaliti ndugu auawe, baba atamsaliti mtoto wake. Watoto watainuka dhidi ya wazazi wao na kuwafanya wauwawe. 13 Mtachukiwa na kila mtu kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, mtu huyo ataokoka. 14 Mtakapoliona chukizo la uharibifu limesimama mahali ambapo halipaswi kusimama (asomaye na afahamu), ndipo walioko ndani ya Yudea wakimbilie milimani, 15 naye aliyeko juu ya paa asishuke ndani ya nyumba, wala kuchukua kitu ndani yake, 16 na aliyeko shambani asirudi kuchukua vazi lake. 17 Lakini ole wao wanawake wenye mimba na wanyonyeshao katika siku hizo! 18 Ombeni kwamba isitokee wakati wa baridi. 19 Kwa maana hizo zitakua siku za dhiki kuu, ambayo hajatokea namna yake tangu mwanzo wa kuumba alipoumba mungu, hata sasa, la, wala haitakuwapo tena. 20 Kama Bwana asingalifupisha siku hizo, hakuna mtu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule aliowachagua alifupisha siku hizo. 21 Wakati huo kama mtu yeyote atawaambia, "Tazama, Kristo yuko hapa!' au 'Tazama, yuko pale!' msiamini. 22 Kwani Wakristo wa uongo na manabii wa uongo watatokea na watatoa ishara na maajabu, ili kwamba, wawadanganye, yamkini hata wateule. 23 Iweni macho! Nimekwisha wambia haya yote kabla ya wakati. 24 Lakini baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga wake, 25 nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu zilizoko mbinguni zitatikisika. 26 Ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu kubwa na utukufu. 27 Ndipo atatuma malaika zake na atawakusanya pamoja wateule wake kutoka pande kuu nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu. 28 Jifunzeni kutoka kwa mtini. Mara tu tawi linapoanza kuwa laini na kung'o majani yake, mnajua majira ya kiangazi yamekaribia. 29 Vivyo hivyo, mwonapo mambo hayo yakitendeka, tambueni ya kuwa yeye yu karibu, karibu na malango. 30 Kweli, nawambieni, kizazi hiki hakitapita mpaka mambo haya yote yatukie. 31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 32 Lakini kuhusu siku hiyo au saa, hakuna ajuaye, hata malaika mbinguni, wala Mwana, ila Baba. 33 Kuweni wangalifu, Kesheni, kwa sababu hamjui ni muda gani yatatokea. (Zingatia: Mstari huu, "Muwe waangalifu, Tazameni na ombeni kwa sababu..." haumo kwenye nakala za kale). 34 Ni kama mtu anayeenda safarini: anaacha nyumba yake, na kumweka watuumishi wake kuwa watawala wa nyumba, kila mmoja na kazi yake, Na kumwamuru mlinzi kukaa macho. 35 Kwa hiyo iweni macho! Kwani hamjui ni lini bwana wa nyumba atakaporudi nyumbani, yawezekana ni jioni, usiku wa manane, wakati jogoo atakapowika, au asubuhi. 36 Kama akija ghafla, asikukute umelala. 37 ninachowaambia nawaambia kila mtu, : Kesheni"!