Sura 8

1 (Zingatia: Angalia ufafanuzi wa Yohana 7: 53 - 8: 11 hapo juu). Yesu alienda mlima wa Mizeituni. 2 Mapema asubuhi akaja tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; akakaa na kuwafundisha. 3 Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyekamatwa katika kitendo cha kuzini. Wakamweka katikati. 4 (Zingatia: Angalia ufafanuzi wa Yohana 7: 53 - 8: 11 hapo juu). Ndipo wakamwambia Yesu, "Mwalimu, mwanamke huyu amekamatwa katika tendo la uzinzi kabisa. 5 Sasa, katika sheria, Musa ametuamuru kuwapiga mawe watu kama hawa, unasemaje juu yake? 6 Walisema haya ili kumnasa ili kwamba wapate jambo la kumshitaki, lakini Yesu akainama chini akaandika katika ardhi kwa kidole chake. 7 (Zingatia: Angalia ufafanuzi wa Yohana 7: 53 - 8: 11 hapo juu). Walipoendelea kumwuliza maswali alisimama na kuwaambia, "Yeye asiyekuwa na dhambi miongoni mwenu, awe wa kwanza kumpiga mawe." 8 Akainama tena chini, akaandika katika mchanga kwa kidole chake. 9 (Zingatia: Angalia ufafanuzi wa Yohana 7: 53 - 8: 11 hapo juu). Waliposikia hayo, waliondoka mmoja mmoja, kuanzia aliye mzee. Mwishowe Yesu aliachwa peke yake, pamoja na mwanamke aliyekuwa katikati yao. 10 Yesu alisimama na kumwambia, "Mwanamke, waliokushitaki wako wapi? Hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?" 11 Akasema, "Hakuna hata mmoja Bwana." Yesu akasema, "Hata mimi sikuhukumu. Enenda.kuanzia sasa na kuendelea usitende dhambi tena." 12 Tena Yesu akazungumza na watu akisema, "Mimi ni nuru ya ulimwengu; yeyote anifuataye hatatembea gizani bali atakuwa na nuru ya uzima." 13 Mafarisayo wakamwambia, "Wajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako siyo wa kweli." 14 Yesu alijibu akawaambia, "Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli. Ninajua mahali nilikotoka na kule ninakoenda, lakini ninyi hamjui mahali ninapotoka au kule niendako. 15 Nyinyi mnahukumu kimwili; mimi simhukumu yeyote. 16 Mimi hata nikihukumu, hukumu yangu ni kweli kwa sababu siko peke yangu, bali niko pamoja na baba aliyenituma. 17 Ndiyo, na katika sheria yenu imeandikwa kwamba ushuhuda wa watu wawili ni kweli. 18 Mimi ndiye ninayejishuhudia, na Baba aliyenituma ananishuhudia." 19 Wakamwambia, "Baba yako yuko wapi?" Yesu akajibu, "mimi hamnijui wala Baba yangu hammjui; mngelikuwa mnanijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia." 20 Alisema maneno haya akiwa karibu na hazina alipokuwa akifundisha hekaluni, na hakuna hata mmoja aliyemkamata kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijafika. 21 Basi akawaambia tena, "Ninaenda zangu; mtanitafuta na mtakufa katika dhambi zenu. Kule niendako, hamuwezi kuja." 22 Wayahudi wakasema, "Atajiua mwenyewe, maana anasema,'kule niendako hamuwezi kuja'?" 23 Yesu akawaambia, "Mnatoka chini; mimi natoka juu. Ninyi ni wa Ulimwengu huu; mimi si wa ulimwengu huu. 24 Kwa hiyo, naliwaambieni kuwa mtakufa katika dhambi zenu.Msipoamini kuwa MIMI NDIYE, mtakufa katika dhambi zenu". 25 Kwa hiyo wakamwambia, "Wewe ni nani?" Yesu akawaambia, Yale niliyowaambia tangu mwanzo. 26 Ninayo mambo mengi ya kuzungumza na kuhukumu juu yenu. Hata hivyo, yeye aliyenituma ni wa kweli; na mambo niliyoyasikia kutoka kwake, mambo haya nayasema kwa Ulimwengu." 27 Hawakumuelewa kwamba alikuwa akiongea nao kuhusu Baba. 28 Yesu akasema, "Mtakapomwinua juu Mwana wa Mtu, ndipo mtakapojua kuwa MIMI NDIYE, na kwamba sifanyi lolote kwa nafsi yangu. Kama Baba alivyonifundisha, ninazungumza mambo haya. 29 Yeye aliyenituma yuko pamoja nami, na yeye hajaniacha peke yangu, kwani kila mara nafanya yale yanayompendeza." 30 Wakati Yesu akisema mambo haya, wengi wakamwamini. 31 Yesu akasema kwa wale Wayahudi waliomwamini, "Ikiwa mtakaa katika neno langu, ndipo mtakuwa wanafunzi wangu kweli, 32 nanyi mtaijua kweli, na kweli itawaweka huru." 33 Walimjibu, "Sisi ni uzao wa Ibrahimu na kamwe hatujawahi kuwa chini ya utumwa wa yeyote; utasemaje, "Tutawekwa huru?" 34 Yesu aliwajibu, "Amini, amini, nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai nyumbani wakati wote; mwana hudumu siku zote. 36 Kwa hiyo, ikiwa Mwana atawaweka huru, kabisa mtakuwa huru kweli." 37 Ninajua kwamba ninyi ni uzao wa Ibrahimu; mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halina nafasi ndani yenu. 38 Ninasema mambo ambayo nimeyaona pamoja na Baba yangu, na ninyi vile vile mnafanya mambo ambayo mliyasikia kutoka kwa baba yenu." 39 Walijibu na kumwambia, "Baba yetu ni Abrahamu." Yesu akawaambia, Kama mngelikuwa watoto wa Ibrahimu, mngefanya kazi za Ibrahimu. 40 Hata sasa mnatafuta kuniua, mtu aliyewaambia ukweli kwamba nilisikia kutoka kwa Mungu. Abrahamu hakufanya hivi. 41 Mnafanya kazi za baba yenu." Wakamwambia, "Hatukuzaliwa katika uzinzi, tunaye Baba mmoja, Mungu." 42 Yesu akawaambia, "Ikiwa Mungu ni Baba yenu, mngenipenda mimi,maana nimetoka kwa Mungu; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye alinituma. 43 Kwa nini hamyaelewi maneno yangu? Kwa sababu hamuwezi kuvumilia kuyasikia maneno yangu. 44 Ninyi ni wa baba yenu, shetani, na mnataka kuzitenda tamaa za baba yenu. Alikuwa mwuaji tangu mwanzo na hawezi kusimama katika kweli kwa sababu kweli haimo ndani yake. Anapoongea uongo, anaongea kutoka kwenye asili yake kwa sababu ni mwongo na baba wa uongo. 45 Hata sasa, kwa sababu ninasema iliyo kweli, hamniamini. 46 Ni nani kati yenu anayenishuhudia kuwa nina dhambi? ikiwa ninasema iliyo kweli, kwa nini hamniamini? 47 Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; ninyi hamyasikii kwa sababu ninyi si wa Mungu." 48 Wayahudi wakamjibu na kumwambia, hatujasema kweli kuwa wewe ni Msamaria na una pepo?" 49 Yesu akajibu, sina pepo; lakini namheshimu Baba yangu, nanyi hamniheshimu. 50 Sitafuti utukufu wangu; kuna mmoja atafutaye na kuhukumu. 51 Amini, amini, nawaambia, iwapo yeyote atalishika neno langu, hataona mauti kamwe." 52 Wayahudi wakamwambia, "Sasa tumejua kuwa una pepo. Abrahamu na manabii walikufa; lakini unasema, 'Ikiwa mtu atalishika neno langu, hataonja mauti'. 53 Wewe si mkuu kuliko baba yetu Abrahamu aliyekufa, sivyo? Manabii pia walikufa. Wewe wajifanya kuwa nani?" 54 Yesu akajibu, "Ikiwa nitajitukuza mwenyewe, utukufu wangu ni bure; ni Baba yangu anayenitukuza - yule mnayemsema kuwa ni Mungu wenu. 55 Ninyi hamjamjua yeye, lakini mimi namjua yeye. Ikiwa nitasema, 'simjui,' nitakuwa kama nyinyi, muongo. Hata hivyo, ninamjua na maneno yake nimeyashika. 56 Baba yenu Abrahamu alishangilia alivyoiona siku yangu; aliiona na alifurahi." 57 Wayahudi wakamwambia,"Haujafikisha umri wa miaka hamsini bado, nawe umemuona Ibrahimu?" 58 Yesu akawaambia, "Amini, amini, nawaambia, kabla Abrahamu hajazaliwa, MIMI NIKO." 59 Ndipo walichukua mawe wapate kumpiga, lakini Yesu alijificha na akatoka nje ya hekalu.