Sura 8

1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Belshaza, mimi Danieli niliona maono (baada ya maono ya kwanza yaliyonitokea). 2 Nilipokuwa nikiangalia, niliona katika maono, kwamba nilikuwa katika mji wa Shushani kwenye ngome ya jimbo la Elamu. Niliona katika maono kuwa nilikuwa karibu na mfereji wa Ulai. 3 Nilitazama juu na nikaona mbele yangu kondoo dume lenye pembe mbili, limesimama pembeni mwa mfereji. Pembe moja ilikuwa ndefu kuliko nyingine, lakini pembe ndefu ilikuwa inakua pole pole kuliko ile fupi na pembe fupi ilirefuka na kuizidi nyingine. 4 Niliona kondoo dume akiishambulia magharibi, kisha kaskazini, na baadaye kusini; hakuna mnyama mwingine aliweza kusimama mbele yake. Hakuna yeyote kati yao aliweza kumwokoa yeyote katika mkono wake. Alifanya chochote kile alichokitaka, na akawa mkubwa sana. 5 Na nilipokuwa natafakari juu ya hili, niliona beberu akitoka magharibi, na kuvuka katika uso wa dunia yote, akikimbia kwa kasi kana kwamba haonekani akigusa ardhi. Mbuzi huyo alikuwa na pembe kubwa katikati ya macho yake. 6 Alikuja mpaka kwa kondoo aliyekuwa na pembe mbili--nilikuwa nimemwona kondoo dume amesimama katika ukingo wa mfereji--na mbuzi alikimbia kumwelekea kondoo dume kwa hasira kali. 7 Niliiona mbuzi akija karibu na kondoo. Mbuzi alikuwa na hasira kali dhidi ya kondoo, na alimgonga kondoo na kuzivunja pembe zake mbili. Kondoo hakuwa na nguvu za kusimama mbele zake. Mbuzi alimgonga kondoo kwa kumbwaga chini na kumkanyagakanyaga. Hapakuwa na yeyote wa kumwokoa kutoka katika nguvu zake. 8 Ndipo mbuzi alikua mkubwa sana, lakini alipokuwa na nguvu, pembe kubwa ilivunjwa, na katika sehemu yake zilichipuka na kukua pembe nne kubwa zilizochomoza kuelekea pepo nne za mbingu. 9 Kutoka katika pembe moja ilichipuka pembe nyingine, ilikuwa ndogo hapo awali, lakini baadaye ilikuwa pembe kubwa upande wa kusini, na mashariki, na katika Nchi ya Uzuri. 10 Pembe ilikuwa kubwa kiasi cha kuinua vita dhidi ya jeshi la mbinguni. Baadhi ya jeshi hilo na nyota kadhaa zilitupwa chini duniani, na zilikanyagwa. 11 Alizidi kujifanya mkubwa, kama kamanda wa jeshi. Sadaka za kuteketezwa za kila siku ziliondolewa mbali na yeye, na sehemu yake takatifu ilitiwa unajisi. 12 Kwasababu ya uasi, pembe ya mbuzi itapewa jeshi, na sadaka za kuteketezwa zitasitishwa. Pembe itautupa ukweli chini ardhini, na itafanikiwa katika jambo ilifanyalo. 13 Kisha nilimsikia mtakatifu mmoja akiongea na mtakatifu mwingine akimjibu, " Mambo haya yatadumu kwa muda gani, maono haya kuhusu sadaka ya kuteketezwa, dhambi ile iletayo uharibifu, ukabidhishaji wa mahali patakatifu, na jeshi la mbinguni kukanyagwa? 14 Aliniambia, " Itadumu kwa jioni na asubuhi zipatazo 2, 300. Baada ya hapo, mahali patakatifu patarejeshwa." 15 Wakati mimi Danieli, nilipoona maono, nilijaribu kuyaelewa. Ndipo mbele yangu alisimama yule aliyeoneakana kama mtu. 16 Niliisikia sauti ya mtu ikiita katikati ya kingo za mfereji wa Ulai. Alisema, "Gabrieli, msaidie mtu huyu kuelewa maono." 17 Basi alikuja karibu na mahali niliposimama. Na alipokuja, nilishtuka na nikaanguka kifudifudi hadi chini. Lakini aliniambia, "Fahamu, mwana wa mtu, kwamba maono ni kwa ajili ya wakati wa mwisho." 18 Alipoongea na mimi, nilipata usingizi mzito nikiwa nimelala kifudifudi. Kisha alinishika na kunisimamisha. 19 Akaniambia, "Tazama, nitakuonyesha kile kitachotokea baadaye katika kipindi cha ghadhabu, kwasababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho uliowekwa. 20 Na kuhusu kondoo mme uliyemwona, yule mwenye pembe mbili - ni wafalme wawili wa Umedi na Uajemi. 21 Mbuzi dume ni mfalme wa Ugiriki. Pembe kubwa katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. 22 Na kuhusu pembe iliyovunjika, ambayo katika nafasi yake pembe zingine nne zilichipuka--hizi ni falme nne zitakazoinuka kutoka katika taifa lake, lakini hazitakuwa na nguvu kubwa. 23 Katika siku zijazo za falme hizo, wakati ambapo wahalifu watakuwa wamefikia kikomo chao, mfalme mwenye uso katili, na yeye mwenye akili sana, atainuka. 24 Nguvu zake zitakuwa kuu--lakini si kwa nguvu zake mwenyewe. Atakuwa wa kustaajabisha kwa kile atakachokuwa anakiharibu; atatenda na kufanikiwa. Atawaangamiza watu wenye nguvu na watu watakatifu. 25 Ataufanya udanganyifu usitawi chini ya mkono wake kwasababu ya ujanja wake. atakuwa mashuhuri kwa akili zake mwenyewe. Atawaangamiza watu wengi bila kutegemea. Atainuka pia dhidi ya Mkuu wa wafalme, na atavunjwa, lakini si kwa mkono wowote wa kibinadamu. 26 Maono kuhusu jioni na asubuhi ulizoambiwa ni ya kweli. Lakini uyafunge maono haya, kwa kuwa yanahusu siku nyingi za wakati ujao. 27 Ndipo mimi, Danieli, nilichoka sana na kulala nikiwa dhaifu kwa siku kadhaa. Kisha niliinuka na nikaenda kufanya kazi za mfalme. Lakini nilikuwa nimetishwa sana na maono, na hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa ameyaelewa.