Sura 22

1 "Ndugu na baba zangu, sikilizeni utetezi wangu ambaao nitakaofanya kwenu sasa." 2 Umati uliposikia Paulo akiongea nao kwa kiebrania, wakanyamaza. Akasema, 3 "Mimi ni myahudi, niliyezaliwa mji wa Tarso eneo la Kilikia, ila nilipata elimu katika mji huu, miguuni pa Gamalieli. Nilifundishwa kulingana na njia sahihi za sheria za baba zetu. Mimi ni mwenye wivu wa Mungu, kama ninyi nyote mlivyo leo. 4 Niliwatesa watu wa njia hii hadi kufa; nikawafunga wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. 5 Hata kuhani mkuu na wazee wote wanaweza kutoa ushahidi kwamba nilipokea barua kutoka kwao kwa ajili ya ndugu walio Dameski, kwangu mimi kusafiri kwenda huko. Ilikuwa niwalete watu Yerusalemu wa njia ile ili wafungwe na kuadhibiwa. 6 Ilitokea kwamba pale nilipokua nikisafiri nakaribia Dameski, majira ya mchana ghafla nuru kuu ikatokea mbinguni ikaanza kuniangaza. 7 Nikaanguka chini na kusikia sauti ikiniambia, 'Sauli, Sauli kwanini unaniudhi?' 8 Nikajibu, 'wewe ni nani, Bwana?' Akaniambia, 'Mimi ni Yesu wa Nazareti, ambaye wewe unaniudhi.' 9 Wale waliokuwa na mimi waliiona nuru, ila hawakusikia sauti ya yule alie ongea na mimi. 10 Nikasema, 'Nifanye nini, Bwana?' Bwana akaniambia, 'Simama na uingie Dameski; huko utaambiwa kila kitu unachopaswa kufanya.' 11 Sikuweza kuona kwa sababu ya muangaza wa nuru ile, ndipo nikaenda Dameski kwa kuongozwa na mikono ya wale waliokuwa na mimi. 12 Huko nikakutana na mtu aitwaye Anania, alikuwa mtu aliyeshika sheria na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote walioishi huko. 13 Akaja kwangu, akasimama mbele yangu, na kusema, 'Ndugu yangu Sauli, upate kuona. 'Kwa muda ule ule nikamuona. 14 Ndipo akasema, 'Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, kumuona yule mwenyehaki, na kusikia sauti itokayo kwenye kinywa chake. 15 Kwa sababu utakuwa shahidi kwake kwa watu wote juu ya uliyoyaona na kusikia. 16 Basi sasa kwa nini unasubiri? Amka, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.' 17 Baada ya kuwa nimerejea Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, ikatokea kwamba nikapewa maono. 18 Nikamuona akiniambia, 'Hima na utoke Yerusalemu haraka, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako kuhusu mimi.' 19 Nikasema, 'Bwana, wao wenyewe wanajua niliwafunga gerezani na kuwapiga wale waliokuamini katika kila sinagogi. 20 Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, Mimi pia nilikuwa nimesimama karibu na kukubali na nilikuwa nalinda nguo za wale waliomuua.' 21 Lakini aliniambia, 'Enenda, kwa sababu mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa mataifa."' 22 Walimsikiliza hadi alipotoa kauli hayo. Ndipo baadaye walipaza sauti na kusema, "Mwondoe mtu huyu katika nchi: kwa sababu sio sahihi aishi." 23 Walipokuwa wakipaza sauti, na kutupa mavazi yao na kutupa mavumbi juu, 24 nahodha mkuu akaamuru Paulo aletwe ngomeni. Akaamuru aulizwe kwa kupigwa mijeledi, ili kwamba, yeye mwenyewe ajue ni kwa nini walikuwa wanampigia kelele namna ile. 25 Hata walipokuwa wamemfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliye simama karibu naye, "Je! ni haki kwenu kumpiga mtu aliye Mrumi na bado hajahukumiwa?" 26 Yule akida aliposikia maneno haya, akaenda kwa jemedari mkuu na kumwambia, akisema, "Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni Mrumi." 27 Jemedari mkuu akaja na kumwambia, "Niambie, je wewe ni raia wa Rumi?" Paulo akasema, "Ndiyo." 28 Jemedari akamjibu, "Ni kupitia kiasi kikubwa cha pesa ndipo nilipata uraia." Lakini Paulo akamwambia, "Mimi ni mrumi wa kuzaliwa." 29 Basi wale waliokuwa tayari kwenda kumuuliza wakaondoka na kumwacha wakati huo huo. Na jemedari naye akaogopa, alipojua kuwa Paulo ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga. 30 Siku iliyofuata, jemedari mkuu alitaka kujua ukweli kuhusu mashtaka ya Wayahudi dhidi ya Paulo. Hivyo akamfungua vifungo vyake na akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza lote wakutane. Akamleta Paulo chini, na kumweka katikati yao.