Sura 14

1 Yoabu mwana wa Seruya akatambua kwamba moyo wa mfalme ulitamani kumwona Absalomu. 2 Hivyo Yoabu akatuma neno huko Tekoa kumleta kwake mwanamke mwerevu. Akamwambia, "Tafadhali, vaa mavazi ya uombolezaji ujifanye kuwa mwombolezaji. Usijipake mafuta, lakini uwe kama mwanamke ambaye ameomboleza kwa muda mrefu kwa ajili yake aliyekufa. 3 Kisha ingia kwa mfalme na umwambie maneno nitakayokueleza." Hivyo Yoabu akamwambia maneno ambayo angeyasema kwa mfalme. 4 Wakati mwanamke kutoka Tekoa alipoongea na mfalme, aliinamisha uso wake chini na kusema, 5 "Mfalme, nisaidie." Mfalme akamwambia, "Shida yako ni nini?" Akajibu, Ukweli ni kwamba mimi ni mjane, mme wangu alikufa. 6 Mimi, mtumishi wako, nilikuwa na wana wawili, wakagombana shambani, na hakukuwa na wa kuwaachanisha. Mmoja wao akampiga mwenziwe na kumwua. 7 Na sasa ukoo wote umeinuka juu ya mtumishi wako, wanasema, 'Mtoe aliyempiga nduguye, ili tumuue kulipa uhai wa nduguye aliyeuawa.' Na hivyo watamwangamiza mrithi. Hivyo watalizima kaa liwakalo nililobakisha, hata kumwondolea mme wangu jina na uzao juu ya uso wa nchi." 8 Hivyo mfalme akamwambia mwanamke, "Nenda nyumbani kwako, nami nitaagiza jambo la kukufanyia." 9 Mwanamke kutoka Tekoa akamjibu mfalme, "Bwana wangu mfalme, hatia na iwe juu yangu na juu ya familia ya baba yangu. Mfalme na kiti chake cha enzi hawana hatia." 10 Mfalme akasema, "Yeyote atakayekwambia neno umlete kwangu, naye hatakugusa tena." 11 Kisha mwanamke akasema, "Tafadhali mfalme amkumbuke Yahwe Mungu wake, ili kwamba mlipa kisasi cha damu asiaribu zaidi, ili kwamba wasimwangamize mwanangu." Mfalme akajibu, "Kama Mungu aishivyo, hakuna hata unywele mmoja wa mwanao utaanguka chini." 12 Kisha mwanamke akasema, "Tafadhali acha mtumishi wako anene neno moja zaidi kwa bwana wangu mfalme." Akasema, "Sema." 13 Hivyo mwanamke akasema, "Kwa nini basi umetenda kwa hila dhidi ya watu wa Mungu? Maana kwa kusema hivi, mfalme ni kama mtu mwenye hatia, kwa kuwa mfalme hamjamrudisha tena mwanaye aliyeondoka. 14 Kwa maana sisi sote tutakufa, kwa kuwa tu kama maji yamwagwayo juu ya ardhi na kwamba hayawezi kukusanywa tena. Lakini Mungu hatachukua uhai; badala yake, utafuta njia kwa walio mbali kurejeshwa. 15 Sasa basi, nimesema jambo hili kwa bwana wangu mfalme, kwa sababu watu wamenitisha. Hivyo mtumishi wako akajinenea nafsini mwake, 'Sasa nitaongea na mfalme. Huenda mfalme akampa mtumishi wake haja yake. 16 Kwa maana mfalme atanisikiliza, ili kwamba kumtoa mtumishi wake katika mikono ya mtu ambaye angeniangamiza mimi na mwanangu pamoja, tutoke katika urithi wa Mungu. 17 Kisha mtumishi wako akaomba, 'Yahwe, tafadhali ruhusu neno la bwana wangu mfalme linipe msaada, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu kwa kutofautisha wema na ubaya.' Yahwe, Mungu na awe pamoja nawe." 18 Ndipo mfalme akajibu na kumwambia yule mwanamke, Tafadhali usinifiche neno lolote nikuulizalo." Mwanamke akajibu, "Basi bwana wangu mfalme na aseme sasa. 19 Mfalme akasema, Je siyo mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu na kusema, "Kama uishivyo bwana wangu mfalme, hakuna awezaye kuelekea mkono wa kulia wala wa kushoto kwa yale bwana wangu mfalme aliyosema. Ni mtumishi wako Yoabu aliyeniambia na kuniagiza kusema kile mtumishi wako alichokisema. 20 Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadilisha hali ya kile kinachotendeka. Bwana wangu ni mwenye akili kama hekima ya malaika wa Mungu, ajuaye yote yatendekayo ndani ya nchi." 21 Hivyo mfalme akamwambia Yoabu, "Tazama, nitatenda jambo hili. Nenda na umrudishe huyo kijana Absalomu." 22 HivyoYoabu akainamisha uso wake chini juu ya ardhi katika heshima na shukrani kwa mfalme. Yoabu akasema, "Mtumishi wako amejua kwamba amepata neema mbele zako, bwana wangu, mfalme, kwa vile mfalme amempa mtumishi wake haja ya moyo wake. 23 Hivyo Yoabu akainuka na kwenda Geshuri, akamrejesha Absalomu Yerusalemu tena. 24 Mfalme akasema, "Na arudi nyumbani kwake, lakini hasinione uso wangu." Hivyo Absalomu akarudi katika nyumba yake mwenyewe, na hakuweza kuuona uso wa mfalme. 25 Hakukuwa na mtu katika Israeli aliyesifiwa kwa urembo wake kama Absalomu. Kutoka katika wayo wa mguu wake hadi katika utosi wake hakuwa na waa lolote. 26 Alipokata nywele za kichwa chake mwishoni mwa kila mwaka, kwa sababu zilikuwa nzito juu yake, alipima nywele zake zaidi ya shekeli mia mbili, kwa kiwango cha kipimo cha mfalme. 27 Kwake Absalomu walizaliwa wana watatu na binti mmoja, jina lake Tamari. Alikuwa mwanamke mzuri. 28 Absalomu akaishi Yerusalem miaka miwili pasipo kuona uso wa mfalme. 29 Kisha Absalomu akatuma neno kwa Yoabu ili ampeleke kwa mfalme, lakini Yoabu hakuenda kwake. Hivyo Absalomu akatuma neno mara ya pili, lakini Yoabu hakuja bado. 30 Hivyo Absalomu akawaambia watumishi wake, "Tazameni, shamba la Yoabu lipo karibu na langu, naye ana shayiri kule. Nendeni mkalichome moto" Hivyo watumishi wa Absalomu wakalichoma moto lile shamba. 31 Kisha Yoabu akainuka na kwenda nyumbani kwa Absalomu akamwambia, "Kwa nini watumishi wako wamelichoma moto shamba langu? 32 Absalomu akamjibu Yoabu, "Tazama nilituma neno kwako kusema, 'Njoo ili nikutume kwa mfalme kusema, "Kwa nini nilikuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningesalia huko. Kwa hivyo sasa niache niuone uso wa mfalme na kama nina hatia basi na aniue." 33 Hivyo Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia. Mfalme alipomwita, Absalomu alikuja kwa mfalme na akainama hadi ardhini mbele ya mfalme na mfalme akambusu Absalomu.