2 Mambo Ya Nyakati Sura 36

1 Kisha watu wa nchi wakamchukua Yehoazi mwana wa Yosia, na wakamfanya mfalme katika nafasi ya baba yake katika Yerusalemu. 2 Yehoazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala, na akatawala miezi mitatu katita Yerusalemu. 3 Mfalme wa Misiri akamwondoa katika Yerusalemu, na akamlazimisha kutoa faini kwa nchi ya talanta za fedha mia moja na talanta moja ya dhahabu. 4 Mfalme wa Misiri akamfanya Eliakimu, ndugu yake, mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu, na akambadilisha jina lake kuwa Yehoakimu. Kisha Neko akamchukua ndugu yake Eliakimu - Yeahazi na kumpeleka Misiri. 5 Yehoakimu alikuwa na umri wa miaka ishini na tano alipoanza kutawala, na akatawala miaka kumi na moja katika Yerusalemu. Akafanya yaliyokuwa maovu katika macho ya Yahwe Mungu wake. 6 Kisha Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akamvamia na kumfunga katika minyororo kumuongoza kwenda mbali Babeli. 7 Nebukadreza pia akabeba baadhi ya vitu katika nyumba ya Yahwe kwenda Babeli, na akaviweka katika ikulu yake huko Babeli. 8 Kwa mambo mengine kuhusu Yehoyakimu, mambo mabaya aliyofanya, na yaliyopatikana dhidi yake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli. Basi Yekonia, mwanaye, akawa mfalme katika nafasi yake. 9 Yekonia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; alitawala miezi mitatu na siku kumi katika Yerusalemu. Akafanya yaliyokuwa maovu katika macho ya Yahwe. 10 Katika kipindi cha mwisho cha mwaka, mfalme Nebukadreza akatuma watu na wakampeleka Babeli,pamoja vitu vya thamani kutoka katika nyumba ya Yahwe, na kumfanya Sedekia ndugu yake, mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu. 11 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na moja katika Yerusalemu. Akafanya yaliokuwa maovu machoni mwa Yahwe Mungu wake. 12 Hakujinyenyekesha mwenyewe mbele za Yeremia nabii, ambaye alisema kutoka kinywani cha Yahwe. 13 Sedekia pia akaasi dhidi ya Mfalme Nebukadreza, ambaye alikuwa amemfanya aape uaminifu kwake kupitia Mungu. Lakini Sedekia aliishupaza shingo yake na kuufanya moyo wake mgumu usigeuke kwa Yahwe, Mungu wa Israeli. 14 Vilevile, viongozi wote wa makuhani na watu hawakuwa waaminifu, na waliufuata uovu wa mataiafa. Wakainajisi nyumba ya Yahwe ambayo alikuwa ameitakasa katika Yerusalemu. 15 Yahwe, Mungu wa babu zao, akatuma maneno kwao tena na tena kupitia wajumbe wake, kwa sababu alikuwa na huruma juu ya watu wake na juu ya sehemu anayoishi. 16 Lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, wakayadharau maneno yake, na kuwackeka manabii wake, hadi hasira ya Yahwe ilipoinuka dhidi ya watu wake, hadi pasiwe msaada. 17 Hivyo Mungu aliwapeleka juu yao mfalme wa Wakaldayo, ambaye aliwaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu, na hakuwa na huruma juu ya vijana au mabikra, watu wazee au wenye mvi. Mungu akawatoa wote mikononi mwake. 18 Vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa na vidogo, hazina za nyumba ya Yahwe, na hazina za mfalme na watumishi wake—vyote hivi akavipeleka Babeli. 19 Wakaichoma moto nyumba ya Mungu, wakauangusha chini ukuta wa Yerusalemu, wakachoma ikulu zake zote, na wakaviaribu vitu vizuri vyote ndani yake. 20 Mfalme akawapeleka mbali Babeli wale waliokuwa wameoka na upanga. Wakawa watumishi wake pamoja na wanawe hadi utawala wa Waajemi. 21 Hili lilitokea ili kulitimiza neno la Yahwe kwa kinywa cha Yeremia, hadi nchi itakapokuwa imefurahia mapumziko ya Sabato yake. Iliishika Sabato kwa muda mrefu hadi kukataliwa kwake, ili miaka sabini itimie katika namna hii. 22 Sasa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Yahwe kwa kinywa cha Yeremia liweze kutimizwa, Yahwe akaipa hamasa roho ya Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwamba akafanya tangazo katika ufalme wake wote, na akaliweka pia katika maandishi. Akasema, 23 "Hivi ndivyo Koreshi, mfalme wa Uajemi, anasema: Yahwe, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia. Ameniagiza nijenge nyumba kwa ajili yake katika Yerusalemu, ambayo ipo Yuda. Yeyote aliyemiongoni mwenu kutoka katika watu wake wote, Yahwe Mungu wenu, awe naye. Akwee kwenye ile nchi."