Sura 40

1 Ikawa baada ya mambo haya, mnyweshaji wa mfalme wa Misri na mwokaji wa mfalme walimkosea bwana wao, mfalme wa Misri. 2 Farao akawakasirikia hawa maafisa wawili, mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji. 3 Akawaweka katika lindo katika nyumba ya kapteni wa walinzi, katika gereza lile Yusufu alimofungwa. 4 Kapteni wa walinzi akamweka Yusufu kuwa mtumishi wao. Walikaa kifungoni kwa muda fulani.

5 Wote wakaota ndoto - mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliokuwa wamefungwa gerezani - kila mmoja akaota ndoto usiku huo huo, na kila ndoto ilikuwa na tafsiri yake.

6 Yusufu akaja kwao asubuhi na kuwaona. Tazama, walikuwa na huzuni. 7 Akawauliza maafisa wa Farao waliokuwa pamoja naye kifungoni katika nyumba ya bwana wake, kusema, “Kwa nini leo mnaoneka wenye huzuni?” 8 Wakamwambia, “Sisi wote tumeota ndoto na hakuna wakuitafsiri.” Yusufu akawaambia, “Je tafsiri haitoki kwa Mungu? Niambieni, tafadhali.” 9 Mkuu wa wanyweshaji akamwambia Yusufu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu, tazama, kulikuwa na mzabibu mbele yangu. 10 Na kulikuwa na matawi matatu katika mzabibu huo. Ulipochipua, ukachanua maua na kuzaa vichala vya zabibu. 11 Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu. Nikachukua zabibu na kuzikamua katika kikombe cha Farao, na kukiweka kikombe katika mkono wa Farao.” 12 Yusufu akamwambia, “Tafsiri yake ni hii. Yale matawi matatu ni siku tatu. 13 Ndani ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako na kukurudisha katika nafasi yako. Utakiweka kikombe cha Farao katika mkono wake, kama ulivyokuwa ulipokuwa mnyweshaji wake. 14 Lakini unikumbuke ukifanikiwa, na unionyeshe wema. Unitaje kwa Farao na kuniondoa hapa gerezani. 15 Maana hakika nilitekwa kutoka katika nchi ya Waebrania. Na hapa sijafanya chochote kinachonipasa niwekwe gerezani.”

16 Mkuu wa waokaji alipoona kwamba tafsiri ilikuwa ya kuvutia, akamwambia Yusufu, “Mimi pia niliota ndoto, na tazama, vikapu vitatu vya mikate vilikuwa juu ya kichwa changu. 17 Katika kikapu cha juu kulikuwa na kila aina za bidhaa ya kuokwa kwa Farao, lakini ndege wakavila ndani ya kikapu juu ya kichwa changu.” 18 Yusufu akajibu na kusema, “Tafsiri ni hii. Vikapu vitatu ni siku tatu. 19 Ndani ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako kutoka kwako na atakutundika juu ya mti. Ndege watakula mwili wako.”

20 Ikawa siku ya tatu ambayo ilikuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Farao. Akafanya sherehe kwa watumishi wake wote. “Akakiinua juu,” kichwa cha mkuu wa wanyweshaji na kichwa cha mkuu wa waokaji, kati ya watumishi wake. 21 Akamrudisha mkuu wa wanyweshaji katika majukumu yake, na akakiweka tena kikombe katika mkono wa Farao. 22 Lakini akamtundika mkuu wa waokaji, kama Yusufu alivyokuwa amewatafsiria.

23 Hata hivyo mkuu wa wanyweshaji hakukumbuka kumsaidia Yusufu. Badala yake, alimsahau.